Tuesday, April 21, 2015

Tanzania yashiriki mkutano wa ushirikiano wa Afrika na Asia unaofanyika Indonesia

Mhe. Dkt. Mary M. Nagu (Mb) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Uratibu na Mahusiano akichangia hoja katika moja ya mijadala kwenye Mkutano wa Kuadhimisha miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Bara la Asia na Afrika unaoendelea jijini Jakarta nchini Indonesia kuanzia tarehe 19 hadi 24 Aprili 2015. Kulia kwa Waziri ni Mhe. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake ya kudumu nchini Malaysia, Bw. Khatibu Makenga, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Bw. Dismas Assenga, Afisa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia.
Mkutano huo kwa ngazi ya Mawaziri ukiendelea.
==============================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika kufanyika Indonesia

Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika pamoja na Miaka 10 ya Mkakati Mpya wa Ubia Kati ya Asia na Afrika umeanza tarehe 19 Aprili 2015 hapa Jakarta, Indonesia.

Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kinachojadili maazimio mbalimbali yaliyofikiwa mwaka 2005 pamoja na kutengeneza Agenda za Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali kuanzia tarehe 19 mpaka 24 Aprili 2015.

Kaulimbiu ya mkutano huu ni Kupanua wigo wa Ushirikiano kwa nchi wanachama “Advancing South - South Cooperation”.

Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili kwa kina na kupitisha maazimio yatakayodumisha ushirikiano miongoni kwa nchi wanachama katika masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na Afrika na Azimio la Palestina. Maazimio yote hayo matatu yalijadiliwa na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali za nchi wanachama na kisha kupitishwa na Mkutano wa Mawaziri.

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali utafanyika tarehe 22 na 23 Aprili 2015, ambapo Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo anatarajiwa kuufungua kwa kutoa hotuba kwa wageni kabla ya kupitisha na kusaini Maazimio tajwa hapo juu.

Aidha, pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia watajadili mustakabali mzima wa masuala mbalimbali yanayoendelea duniani katika Nyanja ya usalama, ubaguzi wa rangi, matabaka baina ya jamii, usafirishaji haramu wa binadamu, ugaidi na mengineyo. Siku ya mwisho, Mkutano unatarajia kukamilika kwa Wakuu wa nchi na Serikali kutembele jiji la kihistoria la Bandung ambako ndiko ulifanyika Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika miaka 60 iliyopita.

Ujumbe wa Serikali ya Tanzania kwenye mkutano huo, uliongozwa na Mheshimiwa Dkt Mary M. Nagu (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Balozi, Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake nchini Malaysia pamoja na Maafisa wengine katika taasisi hizo. 

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
Tarehe 21 Aprili, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.