Mkutano huo kwa ngazi ya Mawaziri ukiendelea. ==============================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika
kufanyika Indonesia
Mkutano wa Maadhimisho
ya Miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika pamoja na Miaka 10 ya Mkakati
Mpya wa Ubia Kati ya Asia na Afrika umeanza tarehe 19 Aprili 2015 hapa Jakarta,
Indonesia.
Mkutano huo
umetanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kinachojadili maazimio mbalimbali
yaliyofikiwa mwaka 2005 pamoja na kutengeneza Agenda za Mkutano wa Ngazi ya
Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali kuanzia tarehe 19 mpaka 24 Aprili 2015.
Kaulimbiu ya
mkutano huu ni Kupanua wigo wa Ushirikiano kwa nchi wanachama “Advancing South - South Cooperation”.
Lengo kuu la mkutano
huu ni kujadili kwa kina na kupitisha maazimio yatakayodumisha ushirikiano
miongoni kwa nchi wanachama katika masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha
Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na Afrika na Azimio la Palestina. Maazimio
yote hayo matatu yalijadiliwa na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali za nchi
wanachama na kisha kupitishwa na Mkutano wa Mawaziri.
Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali utafanyika tarehe
22 na 23 Aprili 2015, ambapo Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko
Widodo anatarajiwa kuufungua kwa kutoa hotuba kwa wageni kabla ya kupitisha na
kusaini Maazimio tajwa hapo juu.
Aidha, pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia
watajadili mustakabali mzima wa masuala mbalimbali yanayoendelea duniani katika
Nyanja ya usalama, ubaguzi wa rangi, matabaka baina ya jamii, usafirishaji
haramu wa binadamu, ugaidi na mengineyo. Siku ya mwisho, Mkutano unatarajia kukamilika
kwa Wakuu wa nchi na Serikali kutembele jiji la kihistoria la Bandung ambako
ndiko ulifanyika Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika miaka
60 iliyopita.
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania kwenye mkutano huo,
uliongozwa na Mheshimiwa Dkt Mary M. Nagu (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu, Balozi, Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na
Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa
Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake nchini
Malaysia pamoja na Maafisa wengine katika taasisi hizo.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
Tarehe 21 Aprili, 2015
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.