Matembezi yakiendelea. ==================================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa
Wakuu wa Nchi wa Asia na Afrika umemalizika leo hapa jijini Jakarta, Indonesia kwa
kushuhudia kupitishwa maazimio muhimu
matatu ambayo ni kudumisha ushirikiano miongoni kwa nchi wanachama katika
masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na
Afrika na Azimio la Palestina.
Mkutano huo
pia uliadhimisha miaka 60 ya Ushirikiano baina ya nchi za Asia na Afrika pamoja
na miaka 10 ya Mkakati Mpya wa Ubia wa Pamoja kati ya nchi za Asia na Afrika (commemoration of the
60th Anniversary of the Asian-African Conference and the 10th Anniversary of
the New Asia-Africa Strategic Partnership).
Lengo la
maazimio hayo ni kuongeza ushirikiano zaidi kwa kuzileta pamoja nchi wanachama
katika kushughulika changamoto wanazokabiliwa nazo kama vile ukosefu wa amani,
ubaguzi wa rangi, matabaka katika jamii, ukosefu wa chakula, ukosefu wa ajira,
biashara haramu ya kusafirisha binadamu, ugaidi, biashara isiyo na usawa,
uharamia, ujangili pamoja na mengineyo.
Katika hotuba
fupi zilizotolewa na nchi wanachama, nyingi zimeunga mkono suala la taifa la Palestina
kupata uhuru wake, kuendelea kushinikiza mageuzi katika Umoja wa Mataifa
hususan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuweka mazingira mazuri
ya kuwezesha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Afrika na Asia kwa kuimarisha
miundombinu kama vile viwanja vya ndege,
njia za mawasiliano, uzalishaji wa nishati ya kutosha, ujenzi wa reli na
barabara pamoja kuweka masharti rahisi katika kufanya biashara.
Masuala
mengine ni kuachana na utegemezi wa Mashirika ya fedha ya kimataifa ambayo
hayana mifumo yenye usawa, kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali, kuongeza ajira na
elimu kwa vijana na mengineyo.
Aidha, kwa
msukumo sawa na ule unaofanywa na nchi wanachama katika kuisemea Palestina
ipate uhuru wake, nchi hizo pia zimeombwa ziweke nguvu sawa na hiyo katika
kufanikisha upatikani wa uhuru wa nchi ya Sahara Magharibi.
Mkutano huo
umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Asia na Afrika ambapo upande wa Asia
alikuwepo Mwenyeji wa Mkutano Rais wa Indonesia, Mfalme wa Jordan, Rais wa
China, Rais wa Vietnam, Rais wa Iran,
Rais wa Myanmar, Waziri Mkuu wa Japan, Waziri Mkuu wa Thailand, Waziri
Mkuu wa Singapore, Waziri Mkuu wa Bangladesh, Waziri Mkuu wa Malaysia na
wawakilishi wa viongozi wakuu kutoka mataifa mengine ya Asia katika ngazi ya
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Mabalozi.
Kwa upande wa
Afrika alikuwepo Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mfalme wa
Swaziland, Rais wa Madagascar, Rais Siera Leone, Makamu wa Rais wa Afrika ya
Kusini na wawakilishi wa viongozi wakuu wa Nchi za Afrika katika ngazi ya
Mawaziri na Mabalozi. Tanzania
iliwakilishwa na Mhe. Dkt. Mary Nagu (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu
na Mahusiano.
Aidha, Wakuu
wa Nchi na wawakilishi wa Bara la Asia na Afrika walipata fursa ya kuutembelea
mji wa kihistoria wa Bandung ikiwa ni kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya
Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika. Mkutano wa kwanza wa
Wakuu wa Nchi wa Afrika na Asia ulifanyikia katika mji wa Bandung mwaka 1955
ambapo wakuu wa nchi na wawakilishi kutoka nchi 29 zikiwemo nchi saba kutoka
Afrika walihudhuria.
Nchi
kutoka Afrika zilikuwa ni Algeria, Misri, Ethiopia, Ghana, Liberia, Libya na
Sudan ambazo kwa pamoja na zile za Asia walitoka na maazimio kumi katika
mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binadamu kama ambavyo Umoja wa
Mataifa unataka, kuheshimu uhuru wan chi na mipaka yake, kutambua usawa wa
kimatabaka na nchi, kutoingilia kati masuala ya ndani ya nchi nyingine,
kuheshimu haki za kila mtu na mengineyo.
IMETOLEWA
NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
24
APRILI, 2015
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.