|
Membe
awahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na kuwekeza katika Visiwa
vya Comoro
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania
kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji Visiwani Comoro kwani uhusiano
baina ya nchi hizi mbili umeimarika.
Mhe. Membe alitoa
kauli hiyo wakati akilihutubia Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Comoro
lililoandaliwa na Balozi za Tanzania na Comoro kwa kushirikiana na sekta
binafsi za nchi hizo mbili jijini Moroni, Comoro tarehe 23 Aprili, 2015.
“Watanzania tunathaminiwa sana hapa kutokana
na mchango wetu mwaka 2008 tulipokikomboa Kisiwa cha Anjouan kutoka kwa Kanali
Bacar. Sasa Serikali ya Umoja wa Visiwa vya Comoro imeimarika na uhusiano wetu
umeshamiri. Wanatukaribisha sisi kwanza kushirikiana kibiashara, tuchangamkie
fursa hii” alisema Waziri Membe.
Vilevile, Mhe. Membe alisifu jitihada za ofisi za
ubalozi wa nchi hizi mbili kwa kuitikia wito wa kuimarisha uhusiano wa
kibiashara kwa kuandaa kongamano hilo la kihistoria.
“Rais Kikwete alipofanya
ziara yake hapa mwaka 2014, aliahidi kukuza uhusiano wetu na kutoa wito wa
kushirikiana kibiashara kwa manufaa ya nchi zetu. Nawapongeza sana Balozi
Kilumanga na Balozi Fakih kwa kushirikiana na sekta binafsi na kutekeleza hili
kwa wakati”alisema Waziri Membe, ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye
kongamano hilo.
Kwa upande wake, Rais
wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ikililou Dhoinine alisema kuwa yeye na Serikali yake
wanathamini mchango mkubwa wa Tanzania kwa watu wa Comoro na hivyo atahakikisha
uhusiano wetu unakua kwenye nyanja zote, Serikalini, sekta binafsi na hata
baina ya watu wa nchi zote mbili.
Aidha, baada ya
ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walikutanishwa na
wenzao wa Comoro kwenye makundi madogo madogo ili kuibua changamoto zinazokwaza
biashara baina ya nchi hizo. Mikutano hiyo inatarajiwa kuibua njia bora zaidi
ya kuwezesha biashara baina yao na kuimarisha uhusiano baina ya watu wake.
Akiwa jijini Moroni, Mhe.
Membe alipata fursa ya kutembelea fukwe za bahari ambazo ni vivutio vikubwa vya
utalii kwenye nchi hiyo ya visiwa akiwa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Alanrif Said
Hussane, Waziri wa Mambo ya Nje wa Visiwa vya Comoro.
Serikali ya Tanzania
ilifungua ofisi zake za ubalozi mwaka 2013 ambapo inawakilishwa nchini humo na
Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Tanzania, mwenye makazi yake Moroni. Kwa
upande wa Serikali ya Comoro ilifungua Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 2014
na inawakilishwa na Mhe. Ahamed El Badaoui Mohamed Fakih Balozi wa Comoro
mwenye makazi yake Dar es salaam.
Kongamano hilo la siku
mbili lililofunguliwa na Mhe. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Comoro,
lilifanyika kwenye ukumbi wa bunge jijini Moroni, mojawapo ya visiwa vitatu
vinavyounda Umoja wa Visiwa vya Comoro, na kuhudhuriwa na wafanyabiashara
takriban mia moja kutoka Tanzania. Visiwa vingine vinavyounda umoja huo wa
Comoro ni Ngazija (Grand Comoro), Anjouan na Moheli huku mji mkuu ukiwa Moroni.
-Mwisho-
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Sehemu ya Wafanyabiashara waliohudhuria Kongamano hilo wakimsikiliza Mhe. Membe |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.