Wednesday, April 29, 2015

Afrika yamuaga Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa pamoja na Mama Salma Kikwete, Waziri wa Ulinzi, Mhe. Hussein Mwinyi (wa tatu kushoto), Mkuu wa Majeshi, Generali Davis Mwamunyange na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ( wa kwanza kushoto) wakisikiliza hotuba ya Waziri Membe (hayupo pichani) wakati wa shughuli za kitaifa za kumuaga Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita zilizofanyika katika Viwanja vya Lugalo Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Aprili, 2015

Waziri Membe akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita wakati wa shughuli za kitaifa za kumuaga zilizofanyika katika Viwanja vya Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe akimpa pole Mjane wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita, Mama Ngeme Mbita.


Mhe. Membe akimpa pole mmoja wa watoto wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita wakati wa shughuli za kitaifa za kuaga mwili zilizofanyika katika Viwanja vya Lugalo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Mama Netumbo Nandi Ndaitwah akiwa ameongozana na Balozi wa Namibia hapa nchini, Mhe.....kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita wakati wa shughuli za kitaifa za kumuaga zilizofanyika katika Viwanja vya Lugalo. 
Mhe. Mama Netumbo Nandi Ndaitwah akimpa pole Mjane wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita, Mama Ngeme Mbita. 
Baadhi ya Wawakilishi wa Serikali ya  Msumbiji nao wakitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Marehemu Generali Hashim Mbita
Waziri wa Ulinzi wa Zimbabwe, Mhe. S. Sekeramayi (kulia)  akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi wa Zimbabwe, Valarios Sibanda (mwenye sare za jeshi) pamoja na Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, Mhe. Edzai Chimonyo (katikati) akiwa na Wawakilishi wengine wakitoa heshima zao za mwisho
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya nae akitoa heshima zake za mwisho huku akiwa ameongozana Katibu Mwenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye. 
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule akiwa ameonozana na Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoa heshima zao za mwisho.
Kiongozi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini ambaye pia ni Balozi wa DRC, Mhe. Juma Halfan Mpango akitoa mkono wa pole kwa watoto wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita
Balozi wa Zambia hapa nchini, Mhe. Judith Kapijimpango nae akitoa pole kwa wafiwa
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga nae akitoa mkono wa pole kwa wafiwa.


...........Matukio mengine kwenye shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Balozi Mbita

Waziri Membe akisaini Kitabu cha Maombolezo
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa nchini wakishiriki shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita
Mwakilishi wa Serikali ya Msumbiji ambaye ni Mwakilishi wa Kamati Kuu wa FRELIMO, Bw. Zaimundo Domingos Pachinuapa akitoa salamu za rambirambi za Serikali hiyo wakati wa shughuli za kitaifa za kuaga mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita


Mwakilishi wa Serikali ya Afrika Kusini ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Nomaindia  Mfeketo akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serkali yake.
Sehemu ya waombolezaji wakifuatilia matukio
Waziri Membe akiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Mama Netumbo Nandi Ndaitwah wakifuatialia hotuba mbalimbali wakati wa shughuli za kumuaga Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita


Viongozi wa Skauti hapa nchini nao walikuwepo kumuaga Brigedia Generali Hashim Mbita
Juu na Chini ni sehemu ya  waombolezaji wakati wa shughuli za kuaga mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita.
Waziri Membe akisalimiana na Mkuu wa Majeshi, Generali Davis Mwamunyange
Jeneza lililobeba mwili wa Marehemu Brigedia Generali Hashim Mbita likiwa limebebwa na Wanajeshi

Picha na Reginald Philip
==============================

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA MHE. BERNARD MEMBE,
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
WAKATI WA SHUGHULI ZA KUMUAGA MAREHEMU BRIGEDIA JENERALI HASHIM MBITA, TAREHE 29 APRILI, 2015





Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu;


Mheshimiwa Benjamin William Mkapa;
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;


Mama Ngeme Mbita

Mke wa Marehemu;

Watoto wa Marehemu;

Wanafamilia;

Mheshimiwa Hussein Mwinyi
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa;

Jenerali Davis Mwamunyange
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi;


Mheshimiwa Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM;



Viongozi Mbalimbali mliopo hapa;

Mabalozi;

Waombolezaji;

Mabibi na Mabwana;



Nianze kwa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Serikali kwa ujumla. Kifo cha Brigedia Jenerali Hashim Mbita ni msiba mkubwa sio kwetu tu hapa Tanzania, lakini pia kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na bara lote la Afrika. 

Nimelazimika kusimama na kuzungumza mbele yenu kwa kuwa pamoja na heshima kubwa aliyoipata kama mwanajeshi na nafasi zingine kubwa alizowahi kushika, lakini pia Mheshimiwa  Hashim Mbita alitumikia Taifa lake kama Balozi wetu katika jiji la Harare nchini Zimbabwe kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2006.

Kama ilivyoelezwa, Mheshimiwa Mbita atakumbukwa zaidi kama Katibu Mtendaji wa Nchi za Mstari wa Mbele (Frontline States) kwa miaka 22 akiwa nguzo muhimu katika harakati za kupinga ukoloni na kupigania Uhuru kwa nchi kadhaa za Kusini mwa Afrika. Iliyokuwa OAU na kwa ridhaa ya Mwalimu Julius Nyerere, Ofisi za nchi za mstari wa mbele ziliweka makao makuu hapa Dar es Salaam ambapo Jenerali Mbita aliitumikia kati ya mwaka 1972 hadi hadi mwaka 1994.  

Ni harakati hizi hizi ndio ambazo zimepelekea Mhe. Mbita kupatiwa tuzo ya “Medali ya Sir Seretse Khama”, tuzo ya Umoja wa Afrika ya “Son of Africa” na pia “The Royal Order of Munhumutapa” iliyotolewa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwaka 2014.

Ingawaje Mhe. Mbita ametutoka lakini Mawazo na uzoefu wake utabaki nasi daima. Kupitia SADC, “The Hashim Mbita Project” ambayo imeandika na kuhifadhi uzoefu, fikra na kazi zake itakuwa ni hazina kubwa ya Mwanajeshi, Mpigania Uhuru na Mwanadiplomasia Mtanzania. Ameiletea heshima nchi yetu na huyu ni Mkombozi wa kweli wa kupigwa mfano.

Tunajivunia utu wake na ndio maana leo, pamoja nasi tunafutwa mchozi na wenzetu.  Naomba kuwatambulisha  kwenu.

·    Kutoka Namibia, Mheshimiwa Netumbo Nandi Ndaitwah, Naibu Waziri Mkuu na pia Waziri wa Mambo ya Nje.

· Uwakilishi kutoka Zimbabwe, Mheshimiwa Dr. Sydney Selelamayi, Waziri wa Ulinzi na Ujumbe wake.

· Uwakilishi kutoka Afrika Kusini, Mheshimiwa Nomaindia Mfeketo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini.

· Kutoka Msumbiji, Mheshimiwa Raimundos Domingos Pachinuapa, Mwakilishi wa Kamati Kuu wa FRELIMO.

Tunashukuru kwa kuweza kujumuika nasi katika msiba huu.

Kwa heshima na taadhima, tunatoa pole kwa familia na Watanzania wote. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mheshimwa Balozi Brigedia Jenerali Hashim Mbita mahala Pema Peponi.


Amina!

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.