Mhe. Membe akipokea Tuzo ya Heshima kwa mchango wake katika kusaidia jamii
Picha na Reginald Philip ================================
Waziri
Membe awaasa vijana nchini kumcha Mungu
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe amewaasa vijana wa Tanzania
kumcha na kumheshimu Mungu kwani wao ndio nguzo ya amani na maendeleo ya nchi.
Waziri Membe ametoa
rai hiyo tarehe 05 Aprili, 2015 katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam
wakati akihutubia mamia ya watu waliofika uwanjani hapo kuadhimisha miaka 15 ya
Tamasha la Pasaka lililoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions.
Mhe. Membe ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha hilo alisema kuwa amani ya nchi inawategemea
kwa kiasi kikubwa vijana wenye uadilifu na wanaomcha Mungu, kwani pasipo
kufanya hivyo ni rahisi kurubuniwa na kujiunga na makundi mabaya na hatari
yakiwemo ya ugaidi.
“Ndugu zangu upo
uhusiano kati ya dini, vijana na amani ya nchi. Ni wajibu wa viongozi wa dini zote na Serikali kuhimiza
vijana sasa waipende dini kwa sababu ndio msingi wa nchi tunayotaka kuijenga na
ni msingi wa uongozi bora na uadilifu ambao utakabidhiwa mikononi mwenu”,
alisema Waziri Membe.
Mhe. Membe aliongeza
kusema kuwa dini zote duniani zimejikita katika kuleta amani na kusisitiza
kuwa vijana wasiende makanisani kwa
ajili ya ndoa, misiba na ibada za wagonjwa pekee bali pia waende kwa lengo la kupata mafundisho ya
kumcha Mungu kwani taifa lenye vijana
wasio waadilifu haliwezi kuwa na
viongozi bora.
Awali akimkaribisha
Waziri Membe kuzungumza, Askofu David Mwasota wa Kanisa la Naioth Gospel
Assembly alisema kuwa anampongeza na kumshukuru Waziri Membe kwa kuwa tayari
wakati wote anapoalikwa kushiriki Tamasha la Pasaka pamoja nao.
“Mhe. Waziri umati
huu umefurahishwa sana na uwepo wako. Tunatambua kuwa unazo kazi nyingi za
kulitumikia taifa na hata familia yako. Lakini umetambua na kuheshimu umuhimu
wa Tamasha la Pasaka na kukubali mwaliko
wetu. Ni kwa upendo wako huo katika kushirikiana na watu katika shughuli
mbalimbali za kijamii ndio uliokusukuma kuacha mambo mengine yote muhimu na
kuja kushirikiana nasi leo, kwa hili tunasema asante sana”, alisema Askofu Mwasota.
Aidha, wakati wa
Tamasha hilo tuzo mbalimbalii zilitolewa ikiwemo Tuzo ya Heshima kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua
mchango wake katika Sanaa, Tuzo kwa Rais Mstaafu, Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Tuzo
ya Heshima kwa Mhe. Membe kwa kutambua mchango wake katika kujishughulisha na
shughuli za kijamii na Tuzo kwa Vyombo mbalimbali vya Habari.
Viongozi wengine wa
Serikali waliohudhuria Tamasha hilo ni pamoja na Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Mhe. Fenella Mukangara, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
Angela Kairuki na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Paul Makonda.
Tamasha la Pasaka
ambalo lilianzishwa rasmi mwaka 2000 huwashirikisha Waimbaji wa Nyimbo za
Injili kutoka nchini na nje ya nchi ambapo Tamasha la mwaka huu limewashirikisha
waimbaji kutoka hapa nchini, Afrika Kusini, Uingereza na Zambia.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.