Saturday, April 25, 2015

Waziri Membe akutana na Rais wa Comoro, ahudhuria hafla ya Muungano Moroni

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akiwa kwenye mazungumzo na Dkt. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Komoro, alipomtembelea Ikulu nchini humo. Katikati ni Afisa Ubalozi Mwadini Jabir, Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Tanzania Moroni, na pia alikua mkalimani wakati wa mazungumzo hayo.

Serikali za Tanzania na Komoro zimekubaliana kuimarisha sekta ya uchukuzi na miundombinu ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa za biashara na chakula baina ya nchi hizo mbili.

Haya yamesemwa kwenye mazungumzo baina ya Mhe. Dkt. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Komoro, na Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, ambapo Mhe. Membe alimpelekea salamu za Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwenye mazungumzo yao walisisitiza ushirikiano wa nchi hizi mbili hususan kwenye eneo la biashara na uchukuzi. Rais Dhoinine alielezea jinsi sekta ya usafiri wa anga ilivyoathirika kutokana na mgogoro nchini Yemen na kwamba ndege za shirika la ndege la nchi hiyo kwenda Comoro na nchi nyingine duniani zimesitishwa. Rais huyo aliongeza kuwa, tegemeo kubwa la wananchi wake hivi sasa ni Tanzania kupitia shirika lake la ndege ATC ambalo kwa sasa linafanya safari nchini humo mara tatu kwa wiki.

“Ni dhahiri wananchi wetu hutegemea sana usafiri wa anga kwa ajili ya kusafirisha bidhaa mbalimbali hata chakula, na hivyo shirika moja la ndege likiacha safari zake Comoro, tunaathirika sana” alisema Rais Dhoinine.

Kwa upande wa Tanzania, Mhe. Membe ambaye alifuatana na Mhe. Christopher Chiiza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayehusika na masuala ya uwekezaji na uwezeshaji, alisema kuwa pindi shirika la ndege la Tanzania litakapoimarika, ndege zake zitakwenda Comoro kila siku ya wiki, kulinganisha na hali ilivyo sasa.

Aliongeza kuwa bidhaa za chakula na biashara ambazo zinaingia Comoro kutoka nchi za Pakistan, Ufaransa na Ukraine, kama vile mchele, sukari na simenti pia zinapatikana nchini Tanzania. Hivyo ni wakati muafaka sasa kwa nchi hizo kuainisha maeneo muhimu ya ushirikiano ili wananchi wake wanufaike.

Mwaka 2014, Serikali za Tanzania na Comoro zilisaini mkataba wa ushirikiano (General Cooperation Agreement) baina ya nchi na nchi, wakati wa ziara ya Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro.

Kufuatia mazungumzo hayo, Mhe. Membe alimthibitishia Rais Dhoinine azma ya Serikali ya Tanzania ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission) ambayo itaharakisha na kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uhusiano baina ya Tanzania na Comoro.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyikia kwenye Ikulu ya Rais jijini Moroni, Waziri Membe alihudhuria hafla ya siku ya taifa ya Tanzania, Muungano Day, iliyofanyikia nyumbani kwa Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Tanzania nchini Comoro tarehe 23 Aprili 2015, kama sehemu ya Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Komoro.

Akihutubia jumuiya ya wanadiplomasia na wajumbe wa kongamano la biashara waliohudhuria hafla hiyo, Mhe. Membe aliweka msisitizo kwa sekta binafsi za nchi hizi kubuni mbinu za kuimarisha sekta za usafiri, utalii na uchukuzi ili kuneemeka na ushirikiano unaosimamiwa na Serikali za nchi hizo.

“Ni matumaini yangu kuwa uhusiano mzuri wa Serikali zetu utasaidia  na kukuza uhusiano wa biashara na sekta binafsi na hatimaye kuimarisha zaidi uhusiano wa watu wetu” alisema Waziri Membe.

Mhe. Membe alikua nchini Comoro kwa ziara ya siku moja ambapo alihudhuria Kongamano la Biashara na kutembelea fukwe za bahari za visiwa hivyo.

MWISHO.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
25 Aprili 2015



Ujumbe wa Mhe. Membe kwenye mazungumzo na  Mhe. Dkt. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Komoro

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.