Sunday, September 27, 2015

Rais Kikwete atangaza agenda ya Wanawake kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba yake huku wajumbe wengine wakisikiliza wakiwemo Mhe. Sofia Simba (Mb.), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto(wa pili kulia). 

Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mama Getrude Mongela aliyeongoza mkutano mkubwa wa wanawake miaka 20 iliyopita Jijini Beijing China. 




Tanzania yatangaza hatua tano za kuendeleza haki za wanawake na usawa wa kijinsia
·      Yaahidi kufanya mabadiliko makubwa ya kisera na kisheria
·      Miongoni mwa Sheria zitakazohusika ni Sheria ya Ndoa na Sheria ya Urithi
·      Ni katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu  - SDG’s
Tanzania imeahidi kuchukua hatua tano muhimu za kutetetea na kuendelea haki za wanawake kati ya sasa na mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa ya kufuta sheria zinazokandamiza wanawake na kutunga sheria za kuleta usawa wa kijinsia, yote katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) mapya kwa manufaa ya wanawake wa Tanzania.
Miongoni mwa hatua hizo itakuwa ni pamoja na kufuta ama kufanya mabadiliko ambayo yanaendeleza vitendo vya kiutamaduni ambavyo kwavyo vinaendeleza ubaguzi wa wanawake kama vile Sheria ya Ndoa, Sheria ya Urithi na kutunga Sheria ya Kukomesha Ukatili dhidi ya wanawake.
Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa Jumapili, Septemba 27, 2015 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipozungumza katika Mkutano wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Akinamama: Dhamira ya Kuchukua Hatua uliohudhuriwa na wakuu wa nchi mbali mbali duniani kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete ameuambia mkutano huo ulioitishwa  kwa pamoja na Jamhuri ya Watu wa China, Denmark, Mexico na Kenya kuwa hatua ya pili ambayo Tanzania inakusudia kuchukua ni kuridhia makubaliano yote ya kimataifa kuhusu haki za akinamama hasa Makubaliano ya Kimataifa Juu ya Kukomesha Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake – Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women (CEDAW).
Hatua nyingine ambazo Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itachukua katika miaka 15 ijayo ili kuhakikisha usawa wa kijinsia nchini ni zifuatazo:
·      Kuendeleza na kuunga mkono upatikanaji wa raslimali fedha zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia kwa mujibu wa Ajenda ya Kugharimia Maendeleo ya Addis Ababa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinatolewa pesa za kutekeleza mipango ya kitaifa na ya Serikali za mitaa za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake.
·      Kuhakikisha utekelezaji wa uwakilishi wa uongozi wa asilimia 50-50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi zote za maamuzi kwenye ngazi zote.
·      Kupatikana na kutumiwa kwa data na habari za ukweli katika utunzi wa sera na utoaji maamuzi ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.
·      Kutunga na utekelezaji mfumo wa uwajibikaji na ufuatiliaji wa haki za kijinsia na haki za akinamama zilizokubaliwa kitaifa na kwenye ngazi ya Serikali za mitaa.
Rais Kikwete pia amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuhusu hatua za kisera na kisheria ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika miaka ya karibuni kujenga usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2004 ambayo yanawapa akinamama nafasi na haki ya kupata, kushikilia, kutumia na kumiliki ardhi.
Hatua nyingine ni kuwapa wanawake nafasi za maamuzi na uongozi katika nyanja za kisiasa na maisha ya umma. Katika kutekeleza hilo, idadi ya wabunge wanawake imeongezeka kutoka asilimia 21.5 ya wabunge wote mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 34.5 mwaka huu, mawaziri wanawake wameongezeka kutoka sita mwaka 2005 hadi kufikia 26 mwaka huu na idadi ya majaji wanawake imeongezeka kutoka wanane mwaka 2005 hadi kufikia 41 mwaka huu.
Rais Kikwete amesema kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kupunguza vifo vya wanawake wakati uzazi, kutunga Sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kuanzishwa kwa uandaaji wa Bajeti inayotilia maanani mahitaji ya wanawake na kuongeza uwezekaji wa kiuchumi wa akinamama kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) yenye kulenga kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa akinamama wafanyao biashara ndogo ndogo na za kati.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

28 Septemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.