Balozi Mulamula akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Korea Kusini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini Mhe. Chung II mara baada ya kumaliza mazungumzo
Picha na Reginald Philip
=============================================
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amempongeza Balozi
wa Jamhuri ya Korea Kusini hapa nchini, Mhe. Chung II kwa kuiwakilisha vyema nchi yake na
kupelekea miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ile ya miundombinu
kukamilika.
Balozi Mulamula alitoa
pongezi hizo leo alipokutana na Balozi Chung II ambaye alifika Wizarani kwa
lengo la kuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Balozi Mulamula alisema
kuwa Jamhuri ya Korea Kusini imekuwa ni miongoni mwa nchi ambazo Tanzania inashirikiana
nazo kwa karibu katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Alieleza kuwa, nchi hiyo
imeshiriki kikamilifu kutekeleza miradi yenye manufaa makubwa kwa
Tanzania katika Sekta mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, biashara na uboreshaji
wa miundombinu.
"Nakupongeza Mhe.
Balozi kwa uwakilishi wako mzuri kwani katika kipindi chote ulichokuwepo nchini
na kupitia Serikali yako umeweza kukamilisha miradi mikubwa ukiwemo ule wa
Daraja la Kikwete lililojengwa katika Mto Malagarasi huko Kigoma” alisema
Balozi Mulamula.
Aidha, alimhakikishia
ushirikiano kutoka Wizarani na Serikalini kwa ujumla kwa Balozi mpya
atakayeteuliwa na nchi hiyo kuja nchini.
Kwa upande wake, Balozi
Chung II ambaye amekuwepo nchini kwa kipindi cha miaka mitatu aliishukuru
Wizara na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano mzuri aliokuwa akiupata wakati
wote wa uwakilishi wake. Pia aliahidi kuendelea kuitangaza Tanzania nchini
kwake ili kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.