Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa akizungumza wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo. Mkutano huo wa siku mbili umefanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Na Mwandishi Maalum, New York
Wanawake na watoto wa kike wanaelezwa kama kundi ambalo bado halijanufaika ipasavyo na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA)
Na kwa sababu hiyo, wito umetolewa kwa nchi Wanahama wa Umoja wa Mataifa, Asasi za Kiraia naTaasisi za Kimataifa kuhakikisha kwamba panakuwep na mikakati na mipango ya ziada yenye lengo la kupunguza pengo la matumizi ya TEHAMA kati ya wanawake na wanaume.
Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa siku mbili wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa ukitathmini utekelezaji wa Teknolojia na Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo, ikiwa ni miaka kumi tangu mchakato wa kuhakisha kuwa jamii inapata fursa ya kupata na kutumia TEHAMA ambayo itakuwa ni jumuishi na yenye gharama nafuu.
Wajumbe wa mkutano huu walikuwa ni Mawaziri wanaohusika na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Monges Lykketofts ni baadhi ya viongozi wakuu waliozungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba yake mbele ya wajumbe wa Mkutano, Balozi Manongi, amesema Serikali inalichukulia kwa umuhimu wa kipekee suala upatikanaji, uboreshaji, usambazaji na matumizi ya TEHAMA kwa wananchi wake.
Akasema katika kuhakikisha kuwa TEHAMA inakwenda na wakati na inawafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu, serikali imekuwa ikishirikiana na kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje.
Akasema kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea, Tanzania ingependa kuona panakuwapo na ushirikiano zaidi na wenye tija baina ya mataifa yaliyoendelea na yanayoedelea hususani katika eneo la uwezeshawaji wa kiteknolojia,raslimali fedha na mafunzo.
Balozi Manongi, na kama iliyokuwa kwa wazungumzaji wengine, amesema ingawa matumizi ya TEHAMA yamekuwa na manufaa makubwa kwa mwanadamu katika Nyanja mbalimbali, lakini pia pamekuwapo na changamoto kadhaa zitokanazo na matumizi mabaya.
Baadhi ya changamoto hizo ni matumizi yasiyo sahihi ya mitandao, ukiwamo uhalifu wa mitandao , ugaidi, uingiliaji wa masuala binafsi ya mtu, ukiukwaji wa maadili, usambazaji wa matamshi ya chuki na misimamo mikali.
Akabainisha pia kuwa pamezuka tabia sugu ( addiction) ya matumizi ya TEHAMA kiasi cha kudhoofisha mahusiano miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.
Kama hiyo haitoshi matumizi sugu ya TEHAMA yamezalisha tatizo jingine la watu kujikuta wakipata magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kwamba wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye TEHAMA pasipo kuishughulisha miili yao.
Mwakilishi huyo wa Tanzania akasema panahitajika juhudi za pamoja katika kuzikabili changamoto hizo na nyingine nyingi.
Wazungumzaji wengi katika mkutano huo pamoja na kubainisha kuachwa nyuma kwa wanawake na watoto wakike katiika matumizi ya TEHAMA, walieleza pia kwamba kundi jingine ambalo nalo halijanufaika na TEHAMA ni watu wenye ulemavu.
Pia ilielezwa wakati wa mkutano huo kuwa ingawa asilimia 40 ya idadi ya watu wote duniani wamepata fursa ya kutumia TEHAMA, bado kuna pengo kubwa baina ya watumiaji kati ya mataifa yanayoendelea na yale yaliyoendelea.
Halikadhalika imebainishwa kwamba kuna pengo pia miongoni wa watumiaji hao kati ya wale wa mijini na vijijini lakini pia uwezo wa kipato nalo ni tatizo linalosababisha siyo kila mtu anakuwa na uweze wa kumudu gharama za matumizi ya TEHAMA.
Baadhi ya wazungumzaji wengine walikwenda mbali Zaidi kwa kueleza kwamba TEHAMA ni muhimu sana kwa utekelezaji wa ajenda mpya ya maendeleo endelevu lakini pia ni muundombinu muhimu ambao hauna tofauti na miundombinu mingine kama vile barabara. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.