Tuesday, March 22, 2016

JK aendelea kusuluhisha Mgogoro wa Libya.

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya amewasili jijini Tunis nchini Tunisia  kushiriki Mkutano wa nane wa nchi Jirani ya Libya. Mkutano huo ulioitishwa na Serikali ya Tunisia ni muendelezo wa jitihada za nchi jirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya. Rais Mstaafu amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman aliposhiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa jijini Tunis, Rais Mstaafu Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, Arab na Afrika wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh aliyemtembelea hotelini kwake. Katika mazungumzo yao, Waziri Messaleh alimpongeza  Rais Mstaafu Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa Libya ambapo alimuelezea hali ya usalama na kisisa ya  Libya na mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo.Mheshimiwa Abdelkader Messaleh Alimhakikishia Rais Mstaafu ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete alimshukuru Waziri Abdelkader Messaleh kwa maelezo aliyompatia na ushirikiano aliomuahidi na kumuelezea matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo madhali nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau wote kuhakikisha mgogoro huo unatatulika ambapo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa hatimaye suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya uko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.


 Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje ya Oman Mheshimiwa Yusuf bin Alawi bin Abdallah mjini Salalah, Oman kuzungumzia mgogoro wa Libya. Katika mkutano wao wamebadilishana mawazo juu ya suluhisho la kudumu la hali ya siasa, usalama na amani nchini Libya.


 Katika Mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona kuwa mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu. Amewakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya ya hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao. Amewakumbusha dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kupawapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto za Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote. 


 Picha ya pamoja.

===================== 
Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa nchi Jirani na Libya, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya (Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj,  wadau wengine wa Libya  pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya iliyoko jijini Tunis. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016. 

Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika utatuzi wa mgogoro wa Libya ameshiriki Mkutano wa Kamati ya Uandishi ya Baraza Maalum la Uandishi wa Katiba ya Libya (Constitution Drafting Assembly) unaoendelea mjini Salalah, Oman. Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yusuf bin Alawi bin Abdallah na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler.

Katika Mkutano huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona kuwa mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu na Amewakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya ya hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao ikiwa ni pamoja na dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kuwapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto za Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote. 

Rais Mstaafu Kikwete pia amepongeza jitihada za Umoja wa Mataifa chini ya Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Kobler za kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya kupitia Mkataba wa Amani wa Libya (Libya Political Agreement) uliotiwa saini tarehe 17 Desemba, 2015 huko Shkirat, Morocco na kuwahimiza wadau wa pande zote za siasa nchini Libya kutekeleza makubaliano hayo ikiwemo kuundwa kwa serikali na kusimikwa kwa serikali hiyo yalipo makao makuu ya nchi hiyo mjini Tripoli mapema iwezekanavyo.

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Afrika amewahakikishia wajumbe hao utayari wa Umoja wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Falme za Kiarabu (Arab League)  na wadau wengine wote kusaidia jitihada za wananchi wa Libya kurejesha hali ya usalama, amani na utulivu nchini Libya.
                                     MWISHO.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.