Kikao
cha Kumi na Nne cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda, 29 Aprili – 1 Mei, 2016
Gisenyi
RWANDA
Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu
ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika kuanzia tarehe 29 – 30
Aprili, 2016, kimekamilika Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta
mbalimbali wameazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi
mbili.
Kikao hicho cha 14 cha ushirikiano
kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka
huu.
Wakati wa ziara hiyo, wakuu hao
walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na kuibua
maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha
wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande
zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi
hao na vilevile kuchangamkia fursa za ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za
wananchi wa pande zote mbili baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.
Kwa upande wake, Balozi Jeanine
Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda na mwenyeji wa kikao
hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo yanayotekelezeka na tarehe za ukomo
kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili kusukuma utekelezaji na kupata matokeo
ya haraka.
Pamoja na mambo mengine, pande
zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama vile
miundombinu ya ushoroba wa kati (central corridor), kuharakisha ujenzi wa reli
ya kati katika kiwango cha kimataifa (standard gauge), kukuza ushirikiano
katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya ndege ya Rwandair na ATCL,
kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo na
ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.
Mkutano huo pia umekubaliana
kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation Committee) kwa
ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika
Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za
Mambo ya Nje za nchi hizo mbili, itakutana kila robo mwaka.
Aidha, Serikali ya Rwanda imeonesha
utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na Watumishi wa Serikali kwa lengo la
kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu nchini kama vile Chuo cha
Diplomasia (CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii
na Wanyamapori (Mweka) na Chuo cha
Usafirishaji (NIT).
Kwa upande wa Tanzania, Serikali
imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya elimu kwa lengo la
kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa mitaala ya elimu ya
tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.
Mkutano ujao wa kumi na tano wa
Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda utafanyika
mwaka 2018, nchini Tanzania.
Mwisho.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Gisenyi, Rwanda
30 Aprili, 2016
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.