===================================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
Uhuru
wa kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuwajulisha wafanyabiashara wa Tanzania na wananchi wote
kwa ujumla kuwa wanaweza kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko
la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuuza bidhaa zao
ndani ya nchi wanachama yaani Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda pamoja na sisi
wenyewe Tanzania .
Wafanyabiashara wanatakiwa
kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya
Jumuiya ambayo yemebainishwa katika Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki kifungu namba 5 ambapo Jumuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha
(The East African Community Customs Union).
Chini ya Itifaki hiyo
wafanyabiashara wa Nchi Wanachama wana uhuru wa kufanyabiashara ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kutozwa ushuru wa forodha ilimradi bidhaa zao
zimezingatia vigezo na kufuata utaratibu ulioainishwa katika Itifaki hii.
Japokuwa Sudan Kusini
imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado fursa za kufanya
biashara nchini humo hazijakamilika. Hii ni kwasababu nchi hiyo imejiunga na
Jumuiya hivi karibuni na hadi hapo itakaporejesha ‘Instrument’ yaani zile hati za kujiunga na Jumuiya baada ya kufuata
utaratibu wa nchi hiyo, ndipo itakuwa mwanachama kamili ambaye atafurahia matunda
haya tunayoyaongelea hapa. Yaani, Sudani
Kusini itaingia kwenye utaratibu wa utekelezaji wa Itifaki na makubaliano
mbalimbali yaliyofikiwa katika Jumuiya.
Ili mfanyabiashara hasa
mdogo aweze kufanya biashara katika Soko la Jumuiya hii anapaswa kufuata
utaratibu ufuatao:
a. Mfanyabiashara/
Msafirishaji anatakiwa kufika kwenye kituo chochote cha forodha kilichopo
mpakani akiwa na bidhaa yake anayotaka kuuza
kwenye Soko la Jumuiya.
b. Akiwa Kituoni hapo, msafirishaji atatakiwa
kupatiwa cheti cha Uasilia wa Bidhaa Kilichorahisishwa (Simplified Certificate
of Origin) ambacho hutolewa bure na ofisi za Mamlaka ya Forodha Tanzania
zilizopo mipakani.
c. Mfanyabiashara
atatakiwa kujaza taarifa zinazotakiwa kwenye cheti hicho kama vile jina kamili la
msafirishaji, anuani, nchi anayotoka, maelezo ya bidhaa na thamani ya bidhaa.
Afisa forodha wa kituo husika atajaza maeneo yanayomhusu na kugonga muhuri
katika cheti hicho.
d. Mfanyabiashara
atatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa wakati akiingia kwenye nchi
mwanachama anapotaka kuuza bidhaa hiyo.
e. Cheti cha uasilia
wa bidhaa ni kwa ajili ya mfanyabiashara mdogo mwenye bidhaa isiyozidi dola za
Kimarekani 2000. Aidha, mfanyabiashara mdogo halazimiki kuwa na wakala wa
Forodha.
f. Mfanyabiashara
mdogo anatakiwa kufuata taratibu zinazohitajika na taasisi nyingine
zinazohusika katika kuruhusu uingizaji / uagizaji wa bidhaa kama vile:
·
Mamlaka
ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA),
·
Shirikia
la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine.
Wizara inatoa wito
kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla iwapo watakutana na vikwazo
visivyo vya kiforodha wakiwa katika Nchi Wanachama, wawasilane na Wizara
kupitia Mawasiliano yaliyoanishwa hapo juu.
Aidha, wafanyabiashara pia
wanaweza kutoa taarifa za vikwazo wanavyokutana navyo kupitia mfumo wa ujumbe
mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ na
kutuma kwenda namba 15539. Vilevile
kwa madereva wa magari makubwa wanaosafirisha mizigo kwenda Nchi Wanachama
utaratibu umewekwa ambapo madereva hao wanaweza kutoa taarifa za moja kwa moja
kwa Jeshi la Polisi kupitia namba 0713631780
iwapo watakutana na vikwazo visivyo vya Kiforodha vya barabarani. Kadhalika wafanyabiashara pia
wanaweza kuwasilisha malalamiko yao juu ya Vikwazo visivyo vya Kiforodha
kupitia tovuti ambayo ni www.tradebarriers.org
Wizara inahimiza
wafanyabiashara kutumia njia halali za kuvusha bidhaa kwenye mipaka ya Nchi
wanachama kwani njia zisizo halali (Njia za panya) hupelekea wafanyabiashara
wengi kudhulumiwa bidhaa au mali zao, kuvamiwa, kuumia na wakati mwingine kuuza bidhaa kwa bei ya
hasara. Watanzania wanaweza kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na bidhaa zao kutolipa ushuru wa forodha ilimradi wamezingatia
taratibu zilizokubalika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, mfanyabiashara atatakiwa kuwa na hati
ya kusafiria pindi anapotaka kuvuka mpaka kwenda Nchi Mwanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.