Semina
kuhusu Maendeleo ya Viwanda
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema kuwa bila ya ujenzi wa
miundombinu ya uhakika, Tanzania haitaweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo ya Mwaka 2025.
Alitoa kauli hiyo leo, wakati
wa semina ya maendeleo ya viwanda iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa China na kufanyika
kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri alisema kuwa
ili miundombinu imara iweze kujengwa nchini, katika mwaka huu wa fedha, Serikali
imetenga kiasi cha Shilingi trilioni 11.8 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo na
kati ya hizo asilimia 46 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. “Asilimia 46 ya
bajeti ya maendeleo ni kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi ya miundombinu
mbalimbali kama barabara, reli ya kiwango cha kimataifa, ununuzi wa ndege na
meli”.
Prof. Mbarawa aliyashukuru
makampuni ya China kwa kuwekeza nchini katika miradi mbalimbali mikubwa lakini
bado alitoa wito kwa makampuni mengine kutoka nchi hiyo kuja kuwekeza kwa wingi hapa nchini.
Aliyashauri makampuni
kutoka nchini China yaje kuingia ubia na makampuni ya hapa nyumbani katika
uendelezaji wa miradi mbalimbali kama ya reli barabara na nishati. Aliendelea
kueleza kuwa ili kuendeleza sekta ya viwanda nchini, tunahitaji msaada wa
mtaji, utaalamu na elimu ya ufundi kutoka kwa marafiki zetu kama nchi ya China.
Aidha, Prof. Mbarawa
alisisitiza umuhimu wa kuboresha kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo
ambayo ndio imeajiri Watanzania wengi hapa nchini. “Sekta ya kilimo imekuwa
ikikua kwa asilimia 4 hadi 5 hapa nchini lakini ukuaji huo haujajikita hasa
katika kiwango cha uzalishaji (productivity)”. Prof. Mabarawa alisema ili watu
wetu waweze kufaidika na kilimo lazima kiwango cha uzalishaji kiboreshwe
na Serikali ya awamu ya tano imejipanga
kulifanyia kazi suala hilo.
Mhe. Waziri alihitimisha
hotuba yake kwa kuahidi kuwa Serikali itazingatia utunzaji wa mazingira
itakapokuwa inatekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyomo kwenye
Mwaka wa Fedha 2016/2017 na miaka mingine itakayofuata.
Akizungumza awali, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba
(Mb) aliishukuru Serikali ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania
kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo. Alirejea dhamira ya Serikali ya Tanzania
ya kushirikiana na China hususan katika Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na
nchi za Afrika (FOCAC). Alisema Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 4
ambazo China itahamishia viwanda vyake ni ushahidi wa wazi kuwa nchi hizi mbili
zina uhusiano mzuri wa kihistoria.
Kwa upande wake, Balozi wa
China nchini Tanzania, Dkt. Lu Youqing alisisitiza
umuhimu wa kukuza sekta ya viwanda hapa nchini. Alisema sekta ya viwanda
ikikua, itapelekea kufikiwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, itaongeza
ajira, mapato ya Serikali na hivyo kuifanya nchi kujitegemea kifedha.
Alimalizia kwa kuihakikishia Tanzania kuwa nchi yake itatimiza yale yote iliyoyaahidi
kwenye Mkutano wa FOCAC uliofanyika Afrika Kusini mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.