Mhe. Waziri Mahiga akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Humphrey Polepole, kulia kwa Mhe. Polepole ni Mkuu wa Wilaya ya Kindononi Mhe. Ally Hapi na Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Ramadhan Madabida.
=================================================
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), ameipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuchangia madawati kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.
Mhe. Majaliwa ametoa pongezi hizo leo wakati wa hafla ya kupokea mchango wa Madawati wa Wizara zilizofanyika katika Shule ya Msingi Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa anaipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya uongozi wa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa juhudi za kuwashirikisha wadau wanaofanya kazi kwa karibu na Wizara hiyo wakiwemo Mabalozi, Watumishi na Jumuiya mbalimbali za kimataifa katika kutekeleza wito wa Serikali na hatimaye kufanisha azma hiyo.
“Nampongeza Balozi Mahiga kwa mbinu alizotumia za kuwashawishi Mabalozi, Watumishi na Jumuiya mbalimbali za kimataifa na hatimaye leo napokea madawati hayo ambayo ni msaada mkubwa kwa wanafunzi wa Wilaya hii ya Temeke ambayo ina idadi kubwa ya watu na wanafunzi pia” alisema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kusema kuwa, Serikali imetekeleza kikamilifu azma ya kutoa elimu bure kwa tija ambapo shule zimefanikiwa kuandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza mwaka huu kuliko ilivyokuwa hapo awali. Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea kumaliza changamoto zilizotokana na ongezeko hilo ikiwa ni pamoja na kuendelea kuongeza madawati, vyumba vya madarasa na kuboresha maslahi ya Walimu.
“Azma ya Serikali ya Elimu bure imekuwa na tija kwani wazazi wameandikisha kwa wingi watoto wao ambapo nimeambiwa shule hii ya Chamazi imeandikisha zaidi ya wanafunzi 700 wa darasa la kwanza, hayo ni mafanikio makubwa na kinachotakiwa ni Serikali kutekeleza mkakati wake wa kumaliza changamoto zilizopo ili kuendana na ongezeko hilo” alisisitiza Waziri Mkuu.
Vilevile Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni ikiwa ni pamoja na kutimiza wajibu wao wa msingi wa kuwapatia chakula, mavazi na vifaa kwa ajili ya kujifunzia.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali bila kujali dini, rangi, kabila wala itikadi za kisiasa kuendelea kuchangia maendeleo ya nchi hususan katika sekta ya elimu ili kuwawezesha watoto wa kitanzania kupata elimu bora.
Awali akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa ili kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli na kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya nchi, Wizara ilihamasika na kuhakikisha inachangia sekta hiyo ya elimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Wakati wa hafla hiyo Wizara ilimkabidhi Waziri Mkuu jumla ya Shilingi milioni mia moja zilizochangwa na Watumishi wa Wizara, madawati 600 kutoka Ubalozi wa Kuwait hapa nchini na mengine 105 kutoka Jumuiya ya Mabohora nchini. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 85 zilikabidhiwa kwa ajili ya kutengeneza madawati kwa ajili ya Shule za Wilaya ya Temeke huku milioni 15 zikipelekwa Wilaya ya Manyoni kwa ajili ya madawati.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.