****************************************************************
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya
Muugano wa Tanzania imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC)
kukaa meza moja na nchi wanachama wa Mkataba wa Roma hususani zile za Afrika
ili kutafuta suluhu ya changamoto na tofauti zilizopo kati ya mahakama hiyo na
wanachama wake.
Tanzania imetoa wito huo siku ya jumatatu kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Taarifa ya Utendaji ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Taarifa ICC imewasilishwa na Rais wa mahakama hiyo Jaji Slivia Fernandez de Gumendi katika kupindi ambacho Jumuiya ya Kimataifa imekumbwa na taharuki baada ya wanachama wawili wa Mkataba wa Roma, Afrika ya Kusini na Burundi kuwasilisha rasmi katika Umoja wa Mataifa kusudio la kujiondoa huku Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa bado haijawasilisha rasmi nia yake hiyo.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika mchango wake amesema, uwepo au kuanzishwa kwa ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji mkono kutoka Afrika. Akasema uungwaji mkono huo ulitokana hasa baada ya nchi hizo za Afrika kukatishwa tamaa na kuvunjika moyo baada ya kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
“Baada ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo, Mahakama hii, ilikuja kuwa chombo cha kutenda haki dhidi ya watu waliojihusisha na vitendo vya kikatili vikiwamo vya ukatili dhidi ya binadamu, uhalifu kivita na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Madhira yasiyoelezeka yaliyotokea Barani Afrika yakaifanya mahakama hii kuwa chombo cha matumaini dhidi ya wale ambao hawakuweza kuguswa au walikuwa juu ya sheria”. Akasema Balozi Manongi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.