Taarifa ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na
Kenya kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Wakuu wa Nchi Mhe. Rais John Pombe
Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri Kenya
Ndugu
waandishi wa habari, mtakumbuka
kuwa tarehe 28 Juni, 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa
taarifa kwa umma kuhusu vikwazo vya kibiashara ambavyo nchi ya Kenya iliweka
katika baadhi ya bidhaa kwa kipindi cha hivi karibuni. Katika taarifa ile,
Serikali ya Tanzania ilibainisha dhamira yake ya kufanya mazungumzo na Serikali
ya Kenya kwa lengo la kumaliza tofauti hizo za kibiashara baina ya nchi hizi
mbili kwa kuzingatia taratibu za kibiashara tulizokubaliana katika Jumuiya yetu
ya Afrika ya Mashariki.
Bidhaa
za Tanzania ambazo ziliwekewa vikwazo na nchi ya Kenya ni unga wa ngano pamoja
na gesi ya kupikia (LPG). Aidha, juhudi za awali za Serikali ya Tanzania kuona
vikwazo hivyo vinaondelewa na Serikali ya Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda.
Hali hiyo ilipelekea Serikali ya Tanzania nayo kuchukua hatua.
Kwa
kuzingatia mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi zetu mbili na kwa
kujali manufaa mapana ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Viongozi Wakuu wa
nchi hizi mbili Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya
walizungumza na kukubaliana kuondoleana vikwazo hivyo maramoja, Vikwazo hivyo
ni;
1. Serikali ya
Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG)
kutoka Tanzania.
2. Serikali ya
Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini Kenya.
3. Serikali za
Kenya na Tanzania kuondeleana vikwazo vyovyote vile ambavyo vinaweza kuathiri
biashara ya bidhaa na huduma kati ya nchi zetu mbili.
4. Sigara ni
kati ya mambo yaliyojadiliwa. Hata hiyo utekelezaji wake utafuata taratibu za
ndani
Hivyo,
Viongozi Wakuu wa nchi zetu mbili waliwaelekeza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Nchi wa Tanzania na Kenya, Mhe. Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) na Dkt. Amina
Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya
Kenya kuutarifu umma kwamba pande zote mbili zimekubaliana kumaliza tofauti
hizo za kibiashara zilizojitokeza hapo awali.
Katika
kutekeleza hilo, Mhe. Waziri Dkt. Amina Mohamed alimwalika Mhe.Waziri Dkt.
Mahiga nchini Kenya tarehe 23 Julai, 2017 ambapo walifanya Mkutano wa Pamoja na
waandishi wa habari kuutangaza uamuzi wa Viongozi Wakuu wa Kenya na Tanzania
kuondoleana vikwazo hivyo maramoja.
Kufuatia
makubaliano haya ya pamoja kati ya nchi hizi majirani ambazo ni waasisi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia, tunapenda kutaarifu kwamba Mataifa haya
mawili yamekubaliana kuunda Tume ya Pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha
tofauti za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi
changamoto za kibiashara kati ya nchi hizi mbili pindi zinapojitokeza. Tume hii
itaongozwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya na kujumuisha
Mawaziri wanaohusika na masuala yaJumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha,
Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi na Utalii wa nchi zote mbili.
Vilevile,
Mawaziri hawa wataunda mfumo wa kupeana taarifa mara kwa mara kuhusu masuala
yenye changamoto za kibiashara kwa lengo la kuepusha kujirudia kwa tofauti kama
hizi. Ni matarajio yetu kuwa uamuzi huu wa pamoja utakuza zaidi mahusiano ya
kibiashara baina ya nchi hizi mbili. Aidha, tunapenda kuwashukuru
wafanyabiashara wa nchi zetu mbili kwa uvumulivu.
MASWALI NA
MAJIBU BAADA YA TAARIFA YA MSINGI
SWALI: Je
ni kwa nini Kenya waliweka vikwazo hivyo hapo awali?
JIBU: Sababu za
awali zilizotolewa na Serikali ya Kenya zilidai kwamba bidhaa hizo hazikidhi
viwango vya ubora wa kimataifa. Hata hivyo, Wataalamu wa Tanzania
wameihakikishia Kenya kuwa bidhaa za unga wa ngano kutoka Tanzania zina ubora
unaokubalika Kimataifa na huuzwa nchi nyingine za Jumuiya ya afrika Mashariki
na Afrika ya Kati. Halikadhalika bidhaa ya gesi ya kupikia (LPG) inakidhi
viwango vya ubora vya Kimataifa
.
SWALI: Nini
msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu tuhuma za baadhi ya wanasiasa wa Kenya
na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Tanzania kuingilia uchaguzi wa Kenya.
JIBU: Tuhuma hizi
hazina ukweli wowote, na hata nilipokuwa nchini Kenya juzi niliona
zimeripotiwa tena na vyombo vya habari vya Kenya. Naomba nikanushe tena kwa
mara nyingine, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
haijawahi, na wala haifikirii kuingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine
tunazoshirikiana nazo ikiwemo maswala ya uchaguzi. Hatujawahi kuingilia
uchanguzi wa Kenya na hututegemei kufanya hivyo kwenye uchaguzi huu na chaguzi
nyingine zozote. Naomba waandishi wa habari, kabla ya kuandika taarifa hizi,
wazihakiki mara mbili, na watutafute kutoa ufafanuzi kabla ya kuwapelekea
wananchi taarifa hizi za kupotosha. Natoa rai, tuwe waangalifu na walaghai wa
nje wanaotaka kutugombanisha. Nichukue pia fursa hii kuwatakia wananchi
wa Kenya uchaguzi mwema wa amani na huru.
SWALI: Je ni kwanini Tanzania inaonekana
kuweka vizingiti vingi vya kibiashara ikilinganishwa na nchi nyingine kwenye
ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika ya kati kwenye siku za hivi karibuni? Je
hii haitakwaza ukuaji wetu wa uchumi kama nchi?
JIBU: Hapana, hata
kidogo. Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara
ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kuendelea, kutokana na biashara ndani ya
bara la Afrika na hususan ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania kwa
siku za hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. John
Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi makubwa kwenye taasisi zetu za bandari na
ushuru yaani TRA. Hatua hizi zinalenga kwenye kuziba mianya iliyokuwepo huko
nyuma ambayo ilisababisha ukusanywaji hafifu wa mapato. Ni wazi sasa mambo
yanaenda kwa uwazi zaidi na ushuru unatozwa na kukusanywa kwa wakati. Tuna
hakika sasa changamoto hizi zimepungua na nchi jirani zitaendelea kufanya
biashara na sisi bila vikwazo.
SWALI: Kabla
ya kuunda hii kamati ya kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni,
Jumuiya ya Afrika Mashariki imekua ikitatua vipi changamoto kama hizi za
kibiashara hususan kwenye nchi zenye ushindani mkubwa kama Kenya na Tanzania?
JIBU: Jumuiya ya
Afrika Mashariki imejiwekea misingi imara na muhimu ya kutatua changamoto pindi
zinapojitokeza. Hivyo ukiacha jopo la wataalam wa Serikalini kuna Baraza la
Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki ambao pia huweza
kupendekeza ufumbuzi wa changamoto mbalimbali kwa wakuu wa nchi ili kutatua
changamoto hizi. Lakini kutokana na ukaribu uliopo baina ya Tanzania na Kenya,
hili la sasa tumelitatua kwa haraka na kwenda mbele zaidi kuunda tume ya
mawaziri wa nchi zetu mbili ili huko baadae tuweze kutatua masuala kama haya
mapema sana kabla ya kuathiri biashara kati ya nchi zetu mbili.
Ni dhahiri kwamba nchi zetu mbili ni jirani na
tunalindwa na Itifaki za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, lakini pia tuna
ushindani kati yetu. Na ili tupate maendeleo ni lazima kuweka ushindani wenye
tija kwa manufaa ya ukanda wetu na wananchi wetu. Japo kuwa Kenya ipo kwenye
kundi la nchi zenye kipato cha kati, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa
na ni hali ya kawaida kwa changamoto kama hizi kujitokeza pindi nchi zinapokuwa
katika ushindani wa kiuchumi.Kwa namna ya pekee naomba kusifu tena hekima za
Viongozi wetu wa Juu kwa kutatua changamoto hizi kwa wakati.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Julai, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.