TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar
Tunapenda kuwafahamisha kuwa warsha ya APRM itafanyika tarehe
24 – 25 Agosti 2017, kwenye hoteli ya “Golden Tulip Boutique”, Zanzibar. Warsha
hiyo itahudhuriwa na Wakurugenzi na maafisa waandamizi toka idara za Mipango na
Sera za Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wapatao 50.
Na pia itakuwa na watoa mada toka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zanzibar
yenyewe, Afrika ya Kusini, Ghana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.
Warsha hiyo inalenga
kujenga uwezo wa Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kuoanisha
(kuunganisha) Mpango Kazi wa APRM na mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, hasa
Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kuleta Maendeleo Na. III.
Na itajadili masuala
yafuatayo: Namna ya kuunganisha Mipango ya Maendeleo ya nchi, Agenda 2063 ya
Umoja wa Afrika, Malengo Endelevu ya Milenia pamoja na Mpango Kazi wa APRM;
Uzoefu wa nchi nyingine za Kiafrika katika kuunganisha Mipango yao ya Maendeleo
na Mpango Kazi wa APRM na Mkakati wa Tathmini na Ufuatiliaji.
Warsha hiyo
inagharamiwa kwa pamoja baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya
Uchumi Barani Afrika pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Mwishoni inatarajiwa
kuwa washiriki wataweza kuunganisha
Mpango Kazi wa APRM na kuonda changamoto za Utawala Bora pamoja na
Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar kwa lengo la kutumia vizuri rasilimali
zilizopo ili kujenga uhusiano kati ya Mipango hiyo pamoja na kukuza uwezo wa
kitaasisi.
Hatua hiyo ni muhimu
sana kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha Taarifa ya kuondoa
changamoto za Utawala Bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Nchi. Na hatimaye
nchi yetu itaweza kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa
changamoto hizo kwenye kikao cha Wakuu wa nchi wanaoshiriki mchakato wa APRM.
Inatarajiwa kuwa, kwa
kutatua changamoto za utawala bora nchi itaweza kuendelea kuwa na amani na
utulivu, kukuza uchumi, kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kuharakisha
Muungano wa Kikanda, na hatimaye kuwaondolea wananchi umaskini.
Tanzania ni mojawapo kati
ya nchi 36 za Afrika zinazoshiriki mchakato wa APRM, nayo imeshawasilisha
Ripoti yake ya kwanza kwa Wakuu Wenza wanaoshiriki mchakato huu mwaka 2013.
Hivi sasa ipo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto
zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Utawala Bora.
Imetolewa
na APRM Tanzania
22 Agosti 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.