Tuesday, April 10, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA POLAND NCHINI 11-13 APRILI 2018

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Poland, Mhe. Prof. Jacek Craputowicz atafanya ziara ya kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 11 hadi 13 Aprili 2018.  Katika ziara hiyo, Prof. Craputowicz pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) Jijini Dar Es Salaam tarehe 12 Aprili 2018.  Viongozi hao watajadili namna ya kuboresha mahusiano na mashirikiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Poland, hususan katika eneo la uwekezaji na biashara.   

Poland ni moja ya nchi zinazounga mkono Sera ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. Katika kuunga mkono Sera hiyo, Serikali ya Poland imetoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 110 kwa Serikali ya Tanzania.

Kati ya fedha hizo, Dola za Marekani milioni 55 zimetumika kujenga kiwanda cha kuunganisha matrekta Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani ambacho kimeshaanza kazi na Dola za Marekani milioni 55 ni kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ya kilimo katika mikoa minane ya Rukwa, Katavi, Manyara, Ruvuma, Dodoma, Shinyanga, Njombe na Songwe.

Prof. Craputowicz na mwenyeji wake watashiriki hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa ofisi ya Ubalozi wa nchi hiyo zilizopo nyumba namba 15, mtaa wa Mtwara, Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Aprili 2018. Poland ilifungua upya Ubalozi wake nchini mwaka 2017 baada ya kuufunga mwaka 2008 na kabla ya hapo nchi hiyo ilikuwa inawakilishwa kutokea Nairobi, Kenya.

Baada ya ufunguzi viongozi hao watafanya mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi hizo saa tano asubuhi. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
 10 Aprili, 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.