TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
VIONGOZI
WA NCHI MARAFIKI WAENDELEA KUTEMBELEA TANZANIA WAKIONGOZWA NA WAZIRI WA
MAENDELEO YA KIMATAIFA WA NORWAY
Waziri wa Maendeleo ya
Kimataifa wa Norway, Mhe. Nikolai Astrup atafanya
ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 27 hadi 30 Novemba 2018.
Wakati wa ziara
yake nchini, Waziri huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ratiba ya Waziri huyo
itahusisha pia mikutano na viongozi wengine wa Serikali wakiwemo Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Phillip Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango na Bw.
Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mikutano
hiyo itajadili namna ya kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Norway hususani
kwenye maeneo ya ukusanyaji wa mapato, mazingira, nishati na kilimo.
Mheshimiwa
Waziri Astrup pia atatembelea Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya
kukagua miradi ya umeme inayofadhiliwa na Serikali ya Norway ikiwemo iliyoanzishwa
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mtambo wa kuzalisha umeme wa maji
uliojengwa na Norway, Sweden na Finland kwenye miaka ya 1990 na kukarabatiwa
hivi karibuni na Serikali ya Norway. Kwenye ziara mkoani Tanga, Waziri huyo
ataambatana na Mhe. Subira Mgalu (Mb), Naibu Waziri wa Nishati.
Vilevile, Waziri
huyo pamoja na Mhe. Omary Mgumba (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo watatembelea
maghala na mtambo wa kuhifadhi mbolea uliopo karibu na Bandari ya Dar es
Salaam, unaomilikiwa na kampuni ya Yara kutoka Norway ambapo Waziri kutoka
Norway atasaini makubaliano na uongozi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
ambapo Norway itasaidia Programu inayoitwa Farm
to Market Alliance (FtMA) iliyo chini ya WFP.
Ratiba ya Waziri huyo itahusisha
pia hafla itakayojumuisha watanzania waliowahi kusoma na kufanya kazi nchini
Norway. Akiwa ni mmoja wa viongozi waliosoma nchini Norway, Mhe. Job Y. Ndugai
(Mb), Spika wa Bunge la Tanzania atakuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo
inayotegemewa kuhusisha washiriki wapatao 400.
Viongozi wengine wanaotarajiwa
kufanya ziara nchini kati ya tarehe 27 na 30 Novemba 2018 ni Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Gorge
Arreaza tarehe 29 Novemba 2018, Katibu Mkuu anayesimamia maendeleo na
ushirikiano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Dernmark, Bw. Trine Rask tarehe 28
hadi 30 Novemba 2018 na Mkurugenzi anayesimamia nchi za Kusini mwa Jangwa la
Sahara kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi, Balozi Anne Lugon- Moulin
tarehe 27 hadi 29 Novemba 2018. Ziara hizi zinalenga kuongeza wigo wa
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo rafiki.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki
Tarehe
26 Novemba 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.