TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Kampuni kubwa za uwekezaji kutoka Austria na India
Ujumbe
wa Makampuni 16 makubwa ya uwekezaji kutoka Austria utafanya ziara ya kikazi hapa
nchini kuanzia tarehe 28 hadi 30 Januari, 2019.
Ziara
ya ujumbe huo nchini ni mwendelezo wa jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani
ambao unawakilisha pia nchini Austria na wadau mbalimbali katika kutekeleza
diplomasia ya uchumi. Pamoja na mambo
mengine, diplomasia ya uchumi inalenga kwenye kutafuta na kuleta wawekezaji
wenye nia ili wawekeze katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kukuza
uchumi na kuinua kipato cha wananchi.
Makampuni
hayo ya Austria yana nia ya kuangalia fursa za uwekezaji hapa nchini katika
sekta mbalimbali ikiwemo afya, mawasiliano ya simu, umeme wa kutumia maji na
usafirishaji.
Ukiwa
nchini, ujumbe wa Kampuni 8 umeomba kuonana na kufanya majadiliano na viongozi
wa Wizara mbalimbali tarehe 29 Januari, 2019 jijini Dodoma akiwemo Mhe. Japhet
Ngailonga Hasunga (Mb.), Waziri wa Kilimo; Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb.),
Waziri wa Nishati; Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango;
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Lengo
la ujumbe huo kukutana na Mawaziri hao ni kutaka kufahamu kuhusu kazi na miradi
mbalimbali inayosimamiwa na kutekelezwa na wizara hizo ili waone namna ya
kuwekeza katika maeneo hayo.
Aidha,
ujumbe huo utashiriki kwenye Kongamano la Biashara lililoandaliwa kwa
ushirikiano kati ya Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda
Tanzania (TCCIA) na Ubalozi wa Austria. Kongamano hilo litafanyika kwenye
Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam tarehe 28 Januari 2019.
Serikali ya Tanzania na Austria zina mahusiano
ya kidiplomasia ya muda mrefu tangu uhuru ambapo Austria imeendelea kutekeleza
miradi mbalimbali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) hapa nchini
hususan katika sekta ya kilimo, afya na kuwajengea uwezo wanawake. Ziara
ya ujumbe wa makampuni hayo ni dalili njema za kuanza kuimarika zaidi kwa
mahusiano kati ya Tanzania na Austria.
Wakati
huohuo, Ujumbe
wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Bureau
Facility Services Pvt Ltd (CISB) ya
India utafanya ziara hapa nchini kuanzia tarehe 29 Januari hadi 05 Februari
2019. Ziara hiyo ina lengo la kukamilisha utaratibu wa kuwekeza katika maeneo
kadhaa ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha madawa, kutafuta fursa ya kuwekeza kwenye
miundombinu kama vile barabara na madaraja na ujenzi wa nyumba na hoteli.
Wajumbe hao wanatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri na Viongozi
Wakuu Waandamizi wa sekta husika.
Ujumbe
huo wa watu watatu utaongozwa na Bw. Alban Rodricks kutoka CISB ambaye
alishafanya ziara hapa nchini mara kadhaa. Aidha, Ujumbe huo unatarajiwa
kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Hamisi Kigwangala (Mb.), Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb.), Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.
Katika
ziara yao hiyo fursa mbalimbali za kiuwekezaji zinatarajia kuibuliwa pamoja na
kujadiliana namna bora ya kushirikiana kati ya Tanzania na India.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
27 Januari 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.