Sunday, January 27, 2019

Ziara ya Kampuni kubwa za uwekezaji kutoka Austria na India


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Kampuni kubwa za uwekezaji kutoka Austria na India
Ujumbe wa Makampuni 16 makubwa ya uwekezaji kutoka Austria utafanya ziara ya kikazi hapa nchini kuanzia tarehe 28 hadi 30 Januari, 2019.

Ziara ya ujumbe huo nchini ni mwendelezo wa jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambao unawakilisha pia nchini Austria na wadau mbalimbali katika kutekeleza diplomasia ya uchumi.  Pamoja na mambo mengine, diplomasia ya uchumi inalenga kwenye kutafuta na kuleta wawekezaji wenye nia ili wawekeze katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuinua kipato cha wananchi.

Makampuni hayo ya Austria yana nia ya kuangalia fursa za uwekezaji hapa nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, mawasiliano ya simu, umeme wa kutumia maji na usafirishaji.

Ukiwa nchini, ujumbe wa Kampuni 8 umeomba kuonana na kufanya majadiliano na viongozi wa Wizara mbalimbali tarehe 29 Januari, 2019 jijini Dodoma akiwemo Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga (Mb.), Waziri wa Kilimo; Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb.), Waziri wa Nishati; Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango; Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Lengo la ujumbe huo kukutana na Mawaziri hao ni kutaka kufahamu kuhusu kazi na miradi mbalimbali inayosimamiwa na kutekelezwa na wizara hizo ili waone namna ya kuwekeza katika maeneo hayo.


Aidha, ujumbe huo utashiriki kwenye Kongamano la Biashara lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda Tanzania (TCCIA) na Ubalozi wa Austria. Kongamano hilo litafanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam tarehe 28 Januari 2019.

Serikali ya Tanzania na Austria zina mahusiano ya kidiplomasia ya muda mrefu tangu uhuru ambapo Austria imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) hapa nchini hususan katika sekta ya kilimo, afya na kuwajengea uwezo wanawake. Ziara ya ujumbe wa makampuni hayo ni dalili njema za kuanza kuimarika zaidi kwa mahusiano kati ya Tanzania na Austria.

Wakati huohuo, Ujumbe wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Bureau Facility Services Pvt Ltd (CISB) ya India utafanya ziara hapa nchini kuanzia tarehe 29 Januari hadi 05 Februari 2019. Ziara hiyo ina lengo la kukamilisha utaratibu wa kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha madawa, kutafuta fursa ya kuwekeza kwenye miundombinu kama vile barabara na madaraja na ujenzi wa nyumba na hoteli. Wajumbe hao wanatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri na Viongozi Wakuu Waandamizi wa sekta husika.

Ujumbe huo wa watu watatu utaongozwa na Bw. Alban Rodricks kutoka CISB ambaye alishafanya ziara hapa nchini mara kadhaa. Aidha, Ujumbe huo unatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Hamisi Kigwangala (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb.), Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.

Katika ziara yao hiyo fursa mbalimbali za kiuwekezaji zinatarajia kuibuliwa pamoja na kujadiliana namna bora ya kushirikiana kati ya Tanzania na India.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
27 Januari 2019

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.