Shirika la
Fedha Duniani (IMF) limeahidi kuipatia Tanzania fedha itakayoihitaji ili iweze
kuendelea kukabiliana na athari zitokanazo na janga la Covid 19 kwa ajili ya kuimarisha
uchumi wake.
Mkurugenzi
Mkazi wa IMF nchini Tanzania Bw. Jens Reinke ameyasema hayo wakati alipokutana
na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi leo katika ofisi ndogo za wizara jijini
Dar es Salaam.
Pia Bw. Reinke
ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua madhubuti inazozichukua
katika kukabiliana na janga la Covid 19
ili kuepusha madhara ya kiuchumi na kijamii.
Mazungumzo hayo
pia yamelenga miradi ya maendeleo, msamaha wa madeni kwa nchi zinazoendelea
ikiwemo Tanzania, ushirikiano baina ya IFM na Tanzania, biasara na utalii.
Kwa upande
wake, Prof. Kabudi ameishukuru (IMF) kwa msamaha wa madeni ambao umetolewa kwa Tanzania
na nchi nyingine, fedha zitakazoziwezesha nchi hizo kuendelea kukabiliana na Covid
19.
"Tumeongelea
mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano hasa katika kuimarisha uchumi wetu
baada ya janga la covid 19, usirikiano kati ya Tanzania na IMF unafahamika na tumekubaliana
baadhi ya mambo ambayo tutayafanyia kazi kwa kina ili tuweze kuimarisha uchumi wetu
baada ya corona hasa katika sekta ya utalii, biashara na miundombinu,"
amesema Prof. Kabudi.
Katika hatua
nyingine, Waziri Kabudi amekutana
na kumuaga Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Kim Doanh ambaye amemaliza
muda wake wa utumishi na amemtakia maisha mema na kumsihi kuendelea kuwa balozi
mwema kwa Tanzania nchini Vietnam na duniani kwa ujumla.
"Kwa niaba ya Serikali napenda
kukuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Vietnam katika nyanja mbalimbali
za kimataifa ikiwemo kuiunga mkono Vietnum katika kugombea nafasi mbalimbali
katika Masirika ya KImataifa," Amesema Prof. Kabudi.
Nae Balozi Doanh ameishukuru Tanzania
kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia alipokuwa akitekeleza majukumu yake
nchini wakati wote na kuahidi kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili
utaendelea kuimarishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi akisalimiana na Mkurugenzi Mkazi wa IMF nchini Tanzania Bw. Jens Reinke |
Mkurugenzi Mkazi wa IMF nchini Tanzania Bw. Jens
Reinke akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi leo katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es
Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Kim Doanh ambaye
amemaliza muda wake wa utumishi nchini Tanzania
Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Kim Doanh akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi |
Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Kim Doanh akimkabidhi
zawadi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.