Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa
kufanyika tarehe 17 Agosti, 2020 kwa njia ya mtandao (video conference) Ikulu Chamwino
Jijini Dodoma.
Akiongea na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi, Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge amesema mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali utatanguliwa na vikao vya Kamati ya kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu
Wakuu na Mkutano wa Baraza la Mawaziri itakayoanza kufanyika tarehe 10 -13
Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conference).
"Kulingana na taratibu na miongozo ya uendeshaji wa SADC, nafasi ya uenyekiti hushikiliwa na nchi wanachama kwa kupokezana kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Tanzania imekuwa Mwenyekiti tangu Mwezi Agosti, 2019 na inatarajwa kukabidhi Uenyekiti kwa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano huo. Aidha, itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Tanzania ilishika nafasi hii mwaka 2003," Amesema Balozi Ibuge.
Ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa sasa wa SADC, atakabidhi Uenyekiti kwa Mheshimiwa Philipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 17 Agosti 2020 jijini Dodoma kwa njia ya Video Conference.
Balozi
Ibuge ameongeza kuwa, kwa kuwa kwa sasa Kiswahili ni moja kati ya lugha rasmi
za mikutano ya SADC, lugha hiyo itatumika katika ngazi ya Mkutano wa Baraza la
Mawaziri na ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali.
Aidha, Katibu Mkuu, Balozi Ibuge amesema
kuwa, kutokana na janga la COVID-19 na
mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kufanya
mikutano ya ana kwa ana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italazimika kukabidhi
uenyekiti kwa njia ya mtandao ambapo Balozi wa Msumbiji hapa nchini
atakabidhiwa uenyekiti kwa niaba ya nchi yake. Hali kadhalika, Balozi wa
Tanzania nchini Msumbiji atakabidhi Uenyekiti kwa Serikali ya Jamhuri ya
Msumbiji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amesema kuwa mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Miaka 40 ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kukuza Maendeleo na kuhimili Changamoto zinazoikabili Dunia” ambapo kauli mbiu hiyo inatakiwa kutekelezwa na nchi zote Wanachama.
Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC wakiwa katika nchi zao. Nchi hizo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Mauritius, Jamhuri ya Madagascar na Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Zimbabwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea
na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Briedia Jenerali, Wilbert Ibuge akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkutano ukiendelea jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.