TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania yashiriki Mkutano wa SADC wa Troika Mbili na Washirika wa Maendeleo
Dodoma, 21 Novemba 2020
Tanzania imeshiriki Mkutano wa SADC wa Troika Mbili (SADC Double Troika na Washirika wa Maendeleo (International Cooperating Partiners- ICPs) uliofanyika tarehe 19 na 20 Novemba, 2020 kwa njia ya mtandao.
Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kujadili na kutoa maamuzi kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya SADC na Washirikia wa Maendeleo. Yafuatayo ni baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kutolewa maamuzi kwenye mkutano huo: -
1. Mkutano ulipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliotangulia wa SADC/ICPs uliofanyika mwezi Disemba, 2019. Aidha, mkutano huo ulijiridhisha kwa hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ajenda ya ushirikiano wa SADC/ICPs. Miongoni mwa maeneo yaliyotolewa taarifa ya mafanikio ni pamoja na kukutana kwa Kamati Maalum za Wataalam ambazo zimeendelea kudumisha ushirikiano baina ya pande hizo mbili;
2. Mkutano ulipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda (Regional Indicative Strategic Development Plan (RISDP 2020-2030) na Dira ya SADC (yaani SADC Vision-2050); katika ajenda hii SADC iliwasilisha ombi la ufadhili wa utekelezaji wa mpango huo. Aidha, baada ya majadiliano, upande wa ICPs ulikubali kutoa ufadhili kwa ajili ya utekelezaji.
3. Mkutano ulijadili athari za mlipuko wa COVID-19 katika SADC na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kukabiliana na athari hasi za ugonjwa huo; Katika ajenda hii Nchi wanachama ziliomba ICPs kufadhili maboresho ya viwanda vya ndani ambavyo vimejikita katika kuzalisha vifaa tiba, vifaa kinga na madawa na upande wa ICPs ulikubali kuendelea kuifadhili SADC.
4. Mkutano uliijadili taarifa ya maboresho ya ukanda wa kijani (Green Recovery) na mkakati wa SADC wa uchumi wa kijani (SADC Green Economy Strategy). Ushirikiano huu kwa vitendo unahusu hifadhi ya mazingira na uchumi endelevu kama nyenzo ya kufikia maendeleo endelevu katika ukanda wa SADC. Pamoja na mambo mengine masuala yatakayotekelezwa katika eneo hili yanalenga katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa Mazingira katika SADC. Changamoto hizo ni pamoja na uchomaji wa misitu, mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa udongo, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, upotevu wa bioanuai (loss of biodiversity), ukosefu wa ajira, changamoto za kiuchumi na kibiashara zitokanazo na bei ya nishati. mashirikiano katika eneo hili yatajikita katika kugeuza changamoto husika kuwa fursa; na
5. Pamoja na hayo, kikao kilipitia na kujiridhisha utekelezaji wa masuala mtambuka ya ushirikiano kupitia Kamati za Wataalam za Kipaumbele (Thematic Groups) zinazoratibu masuala ya ushirikiano wa ulinzi na usalama, usafirishaji, nishati, maji, udhibiti wa athari za majanga, afya, kilimo, TEHAMA na mabadiliko ya tabia nchi.
Itakumbukwa kuwa, Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulifanyika mwezi Agosti, 2019 Dar es salaam, Tanzania, pamoja na mambo mengine, Mkutano huo ulielekeza itengwe siku maalum ya tarehe 25 Oktoba, 2020 kwa kila mwaka ili kupaza sauti hadi hapo vikwazo kandamizi vya kiuchumi vilivyowekwa nchini Zimbambwe na nchi za Magharibi viweze kuondolewa. Sambamba na hilo, mkutano huo uliagiza Nchi wanachama kupaza sauti katika majukwaa mbalimbali, Kwa namna ya kipekee, Tanzania ilitumia fursa ya mkutano huo, kupaza sauti kwa ajili ya kuondolewa kwa vikwazo kandamizi vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi Jamhuri ya Zimbabwe.
Mkutano huo, uliongozwa na Jamhuri ya Msumbiji ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC kwa kushirikiana na mwenyekiti mwenza kwa upande wa ICPs. Katika Mkutano huo, Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Bi. Agnes R. Kayola, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mkutano kama huo, utaitishwa tena mwaka 2021 kulingana na ratiba na hadidu za rejea za kuendesha vikao vya namna hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.