Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema Tanzania itashirikiana na nchi yoyote duniani ambayo inatambua na kuheshimu Uhuru wa nchi na utu wa watu wake.
Prof. Kabudi ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipozungumza na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zake tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
"Tutafanya kazi na nchi zote ambazo zinatuheshimu, zinatutambua kama Taifa huru, kutuheshimu sisi kama binadamu wa mataifa mengine, hatutakubali kudharauliwa, kutokuheshimiwa utu wetu na kudharauliwa kwa sababu ya misaada au pesa’, amesema Prof. Kabudi
Ameongeza kuwa Tanzania itasikiliza taifa lolote duniani na kujadiliana nalo kwa heshima kwani mapungufu hayapo upande mmoja tu.
"Tuko tayari kuwasikiliza na kujadiliana nao kwa heshima na kama wanadhani kuna kitu kimepungua kwetu na sisi tunadhani kimepungua kwao," amesema Prof. Kabudi.
Amesema Tanzania haiwezi kumruhusu mtu yeyote atumie misaada ya fedha kuondoa uhuru wetu na kutokuthamini utu wetu.
Amesema Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa na itaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kidunia kama vile kulinda amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutunza mazingira.
"Hatutajitenga katika dunia hii, tutaendelea kujumuika katika kazi mbalimbali kama vile ulinzi wa amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuhifadhi mazingira,’ alisema na kuongeza kuwa tumekuwa bandari ya amani kwa wakimbizi sio tu kutoka Afrika bali duniani kote na tutaendelea kuwa hivyo," Ameongeza Prof. Kabudi.
Prof. kabudi pia amewataka watumishi wa Wizara kusoma kitabu cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alichowaandikia watumishi wa wizara hiyo mwaka 1969 cha Usipayuke toa hoja ‘Don’t shout argue’ ili kutoa takwimu sahihi kwa wakati.
Amesema jukumu la kuieleza dunia kuhusu takwimu za vitu mbalimbali ni la watumishi wa Mambo ya Nje na hawana budi kuhakikisha wanaliekeleza hilo kwa ufasaha.
Mbali na kitabu hicho, Prof. Kabudi amewakabidhi wakurugenzi wa Idara mbalimbali Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hotuba za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati anafungu Bunge la 11 na hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 12 na kuwataka kusimamia na kutekeleza maagizo yote yaliyopo kwenye hotuba hizo pamoja na maelekezo ya Ilani ya CCM.
Awali akimkaribisha Waziri kuzungumza na watumishi, Katibu Mkuu Wizara Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wibert Ibuge aliwapongeza watumishi utendaji mzuri wa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akimkabidhi nyaraka Mkurugenzi wa
Kitengo cha Diaspora Balozi, Anisa Mbega |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akimkabidhi nyaraka Kaimu
Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Bibi. Caroline Chipeta |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akiongea na Watumishi wa
wizara katika mkutano uliofanyika jijini
Dodoma |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.