Na Nelson Kessy, Chato
Rais
wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi amewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi na
kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato na kisha kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato.
Akizungunza
katika hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Rufaa
ya Kanda-Chato, Rais Magufuli alimshukuru Rais Mhe. Filipe Nyusi kwa
kumtembelea Chato na kuongeza kuwa
Msumbiji ni rafiki wa muda mrefu wa Tanzania na nchi hizo zina makubaliano ya kushirikiana katika mambo
mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji.
"Biashara
kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka, hadi kufikia mwaka 2020 ilifikia
shilingi bilioni 93.6, kuna makampuni ya Msumbiji yanafanya kazi hapa na baadhi
ya makampuni ya Tanzania yanafanya kazi kule." Amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli ameongeza kuwa Januari 9, 1967 Hayati Mwalimu Julius Nyerere
alitembelea Wilaya ya Chato na kufungua kiwanda cha pamba kilichojengwa kwa
shilingi milioni 2 ambacho kilikuwa na uwezo wa kuchakata marobota 20,000.
Aidha,
Rais Magufuli amesema kuwa Mwalimu Nyerere alichangisha fedha na yeye binafsi
kuchangia shilingi 2,000 kwa ajili ya kujenga bandari ya Nyamirembe ili iweze
kusafirisha pamba kwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa hiyo wa Rais Nyusi amefika
eneo ambalo alifika Mwalimu Nyerere.
"Kwetu
sisi tunaona hii ni zawadi kubwa kwa wewe kuja kuzindua hospitali hii ambayo ni
kubwa na itahudumia pia nchi za jirani.Nawashukuru Wizara ya Afya na
Wakandarasi, nitawabana Wizara ya Afya
ili hospitali hii ikamilike mara moja." Alisema Rais Magufuli
Kwa
upande wake Rais Nyusi amempongeza Rais Magufuli kwa juhudim kubwa za
kushughulikia maisha ya wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha sekta pamoja
na huduma za afya nchini.
"Nashukuru
kwa Rais Magufuli kunipa nafasi ya kuweka jiwe la msingi kwa sababu Serikali
inayoaangalia afya za wananchi hiyo ni Serikali inayopenda wananchi wake. Rais
Magufuli anashughulikia sana maisha ya wananchi wa watanzania kwa kuangalia
nyumba bora za kuishi, huduma za maji, chakula
na afya bora" amesema Rais Nyusi.
"Kwa
hiyo hii ni zawadi kwetu kwa kutupa
nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali hii kubwa, kule Msumbiji
tumeanza (Program ya presidential
initiatives) ya kujenga hospitali kila wilaya hii ni zawadi kubwa kwetu ya kutupa nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika afya ya wananchi," Ameongeza Rais
Nyusi
Aidha,
Rais Nyusi amesema kuwa mkoa wa Geita ni
tajiri kwa kuwa kuna kilimo cha mpunga,
madini ya dhahabu na uvuvi wa
samaki, hivyo kuwataka wananchi wa mkoa huo kufanyakazi kwa bidii.
Naye,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy
Gwajima amesema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda -
Chato ilikadiriwa kutumia sh. bil.16, Serikali imeshatoa sh. bil.14 ambapo
ujenzi umekamilika kwa asilimia 90 na makabidhiano yanatarajiwa kufanyika mwezi
Machi, 2021.
Ameongeza
kuwa awamu ya pili ya ujenzi imeshaanza
kwa jumla ya gharama ya shilingi bilioni 14 ambapo mpaka sasa Serikali imetoa
shilingi bilioni 4.1 na utekelezaji wake umefikia asilimia 37.
"Hospitali
ya Rufaa ya Kanda - Chato itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia
wananchi zaidi ya milioni 14 ambapo kwa siku itakuwa na uwezo wa kuhudumia
wagonjwa kati ya 700 - 1000." Amesema Dkt. Gwajima
Rais
wa Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi yupo nchini kwa ziara ya siku moja ambapo
atafanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu namna ya kuboresha maisha wananchi wetu
pamoja na usalama.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) muda mfupi kabla ya Rais wa
Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi kuwasili katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi wakipita katikati ya
gadi ya heshima mara baada ya Rais Nyusi kuwasili nchini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli na mgeni wake, Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi wakipata maelezo
kuhusu ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato kutoka kwa Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli na mgeni wake, Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi wakimsikiliza maelezo
ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy
Gwajima wakati walipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli na mgeni wake Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi wakiweka rasmi jiwe
la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli akihutubia hadhara ya wananchi (hawapo pichani) mara baada ya kuweka
jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato
Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi akihutubia hadhara ya wananchi (hawapo pichani) mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda - Chato |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Pombe Joseph
Magufuli pamoja na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi wakiwaaga wananchi (hawapo
pichani) mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda
- Chato
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.