Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa Habari Chato mkoani
Geita (Hawapo pichani) kuhusu ziara ya siku mbili ya Rais wa Jamhuri ya
Msumbiji hapa nchini, Mhe. Filipe
Jacinto Nyusi. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge, na kushoto ni Mkuu
wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi. Picha na Nelson Kessy
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa Habari Chato mkoani
Geita kuhusu ziara ya siku mbili ya Rais wa Jamhuri ya Msumbiji hapa nchini, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi. Kulia ni Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia
Jenerali, Wilbert Ibuge, na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert
Luhumbi. Picha na Nelson Kessy
Na Nelson Kessy, Chato
Rais
wa Jamhuri
ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi anatarajia
kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili hapa nchini Tanzania kuanzia tarehe 11 -
12 Januari 2021 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli.
Akithibitisha
juu ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Mhe. Nyusi atawasili nchini kwa ziara
ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika uwanja wa ndege wa Geita -
Chato.
"Ziara hii ya Rais Nyusi ni ziara ya kindugu ambayo ilipangwa
kufanyika muda mrefu lakini haikuweza kufanyika mapema, kutokana na kutokana na
sababu mbalimbali, hususan Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
uliofanyika Oktoba 28, 2020," Amesema Prof. Kabudi.
Aidha,
Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ziara ya Mhe Nyusi, ni kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha
mahusiano ya nchi zetu mbili katika maeneo anuwai, yakiwemo yale ya kidiplomasia,
kiuchumi, kisiasa na kijamii; kama yalivyoasisiwa na vyama vya ukombozi vya
nchi zetu, yaani, chama cha TANU na Chama cha Afro-Shirazi na baadaye Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania na kile cha FRELIMO kwa upande wa
Msumbiji. Mtakumbuka, mahusiano haya yaliyotukuka, yaliasisiwa na viongozi
waanzilishi wa nchi zetu huru, yaani Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanzania na Hayati Dkt. Eduardo Tshivambo
Mondlane kwa upande wa Msumbiji.
"Uhusiano
huo pia umeendelea baada ya Msumbiji kupata uhuru wake kupitia mapambano ya
silaha mwaka 1975, ambapo, kama nyote mnavyofahamu, kuanzia Rais wa Kwanza wa
Msumbiji Huru, Hayati Samora Moises Machel, na wengine wote waliomfuatia hadi
leo, na Marais wa Tanzania baada ya Hayati Baba wa Taifa hadi leo, wote
wameendelea kuimarisha mahusiano hayo na undugu wa Watanzania na Watu wa
Msumbiji ambao kwa hakika ni ndugu wa damu," Ameongeza Prof. Kabudi
Prof. Kabudi ameeleza kuwa,
licha ya uhusiano wa Kihistoria na Kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili, uhusiano
wa Kiuchumi nao umeendelea kuimarika. Tanzania inafanya biashara na Msumbiji
kupitia mazao ya chakula na biashara pamoja na bidhaa za viwandani. Kwa mfano,
takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonesha kuwa jumla ya mauzo
ya Nje (Export) kati ya nchi hizi mbili zilifikia Shilingi za Kitanzania
Bilioni 76.4 kwa mwaka 2018 na Shilingi za Tanzania Bilioni 93.5 kwa mwaka
2019.
Kuhusu uwekezaji, hadi sasa
makampuni makubwa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji ni
pamoja Bakheresa (Azam), Mohammed Enterprises, Quality Foam (Magodoro Dodoma),
n.k. Vilevile kuna Watanzania wanaomiliki kampuni za usafirishaji wa abiria na
mizigo pamoja na biashara za kati na ndogondogo nchini Msumbiji.
"Licha ya changamoto ya
Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) SADC imeendelea kuwezesha na
kusimamia biashara miongoni mwa nchi wanachama. Wakati wa ziara hii viongozi
wetu watabadilishana mawazo ya namna ya kuendelea kuwezesha ufanyaji wa biashara,"
Ameongeza Prof. Kabudi
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi amewataka wananchi wa Geita kujitokeza kwa
wingi na kumpokea mgeni wakati atakapokuwa amewasili katika uwanja wa ndege wa
Geita - Chato.
"Nawasihi wananchi wa
Geita kujitokeza na kumpokea mgeni wetu, kwani hii ni fursa kwa mkoa wetu,
tunapaswa kuitumia fursa hii vizuri" Amesema Mhandisi Luhumbi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.