Friday, February 5, 2021

TZ YATOA MUELEKEO WAKE KATIKA AWAMU YA PILI YA UONGOZI WA RAIS MAGUFULI

Na Mwandishi wetu, 

Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema katika kipindi cha muhula wa pili wa miaka mitano ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli itajikita zaidi katika diplomasia ya uchumi, kuimarisha sekta binafsi, kukuza biashara pamoja na mahusiano na Mataifa mengine duniani. 

Msimamo wa Tanzania umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na Mabalozi wanaoziwakilisha Nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na kuongeza kuwa ni dhamira ya Tanzania kuhakikisha kuwa ina uwezo wa kukuza biashara na kuuza bidhaa katika nchi mbalimbali duniani.

“Katika mwaka huu unaoanza sasa na miaka ijayo katika mhula wa pili awamu ya tano ni wakati muafaka wa Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi na uhusiano mwema baina yake na nchi mbalimbali kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hizo katika maeneno ya uzalishaji, viwanda na kuongeza biashara kwa manufaa ya mataifa yote,” Amesema Prof. Kabudi 

Pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi amewaambia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa Nchini kuwa hali ya kisiasa na amani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imeimarika kuliko wakati wowote hususani mara baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika Octoba, 2020 na kwamba uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar unachochea kuongezeka kwa uwekezaji na ufanyaji wa biashara kwa lengo la kukuza uchumi. 

Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi Dkt. Ahmada El Badasui ambaye pia ni Balozi wa Comoro hapa nchini ameshukuru kwa uwepo wa mkutano huo ambao unawapa fursa mabalozi kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini.

“Nakupongeza Mhe. Waziri na uongozi wa Wizara kwa kuandaa mkutano huu ambao unatupa fursa sisi mabalozi kujadili na kujua mambo mbalimbali yanayoendelea hapa nchini, mikutano kama hii ni muhimu sana kwetu kwani inatusaidia na kutuwezesha kuboresha mahusiano yetu ya kidiplomasia,” Amesema Dkt. El Badasui

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti ameipongeza Tanzania kwa kuingia uchumi wa kati na kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha Uchumi wa Tanzania unaendelea kukua na kuimarika.

Mkutano huo wa Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe William Tate Ole Nasha, Katibu Mkuu Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na vitengo vya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe William Tate Ole Nasha (Mb) akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam


Balozi wa Comoro hapa nchini na kiongozi wa Mabalozi Dkt. Ahmada El Badasui akitoa neno la shukrani kwa viongozi wakuu wa Wizara (hawapo pichani) kabla ya kumalizika kwa mkutano 


Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wakifuatilia mkutano 


Balozi wa Canada Mhe. Pamela O’Donnel akichangia jambo wakati wa Mkutano   


Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Manfredo Fanti akichangia jambo wakati wa Mkutano. Kulia kwake ni Balozi wa Rwanda hapa nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba.  



 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.