Na Mwandishi Wetu
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Jamhuri ya Afrika Kusini zimewasilisha
ombi maalumu kwa Umoja wa Afrika kuzitambua rasmi njia zilizotumika na
wapigania uhuru kutoka Dar es Salaam kupitia nchi mbalimbali Kusini Mwa Bara la
Afrika hadi Namibia kuwa urithi wa Kimataifa.
Ombi hilo limewasilishwa na Rais wa
Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa 34 wa kawaida
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia mtandao na
kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli.
Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika
kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la
Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa
wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni Sanaa, Utamaduni na urithi.
“Tumeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha
ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa
ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru
ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni sanaa, utamaduni na urithi,” Amesema Prof.
Kabudi.
Akiufunga
Mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi amesisitiza kuwa umoja,
mshikamano na amani katika bara la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakayoliwezesha
bara hilo kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali ilizonazo.
“Umoja, mshikamano na amani katika
bara la letu la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakatuwezesha sisi kuendelea
kiuchumi ili kuendana na rasilimali tulizonazo kwa maslahi yetu mapana,” Amesema
Rais Tshisekedi
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo
umejadili mambo mbalimbali ikiwemo uundaji wa Kamati mpya ya uongozi wa Umoja
wa Afrika (the AU Bureau of Assembly) kwa mwaka 2021, uzinduzi wa Kaulimbiu ya
Umoja wa Afrika kwa mwaka 2021 inayohusu “Sanaa, Tamaduni na Urithi katika
kufikia azma ya Afrika Tuitakayo”
Mengine yaliyojadiliwa ni taarifa ya
Maendeleo ya Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu COVID-19 Barani
Afrika, taarifa ya Utekelezaji wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika;
na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ilitumia fursa hiyo kueleza utayari wake kuendelea kushirikiana na
Umoja wa Afrika na Nchi Wanachama wa Umoja huo katika kutekeleza jitihada
zinazolenga kuiwezesha Afrika kujitegemea.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi (Mb) akifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali
wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference ambapo ujumbe wa
Tanzania umehudhuria mkutano huo jijini Dar es Salaam. Kulia mwa Prof. Kabudi
ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge. Prof. Kabudi anamuwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Maafisa mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia Video Conference. Prof. Kabudi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika mkutano huo.
Mkutano ukiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.