Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal Union - PAPU) wenye Makao Makuu yake jijini Arusha, Tanzania Mhe. Younouss Djibrine, alipotembelea Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Dodoma.
Djibrine ameeleza kuwa pamoja na masuala mengine ziara hiyo imelenga kuishukuru Serikali chini ya Uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ushirikiano inayoendelea kuutoa kwa Taasisi hiyo ya Kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Djibrine pia alitumia nafasi hiyo kuelezea hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi mkubwa wa jengo la ofisi za Taasisi hiyo unaoendelea kufanyika jijini Arusha. Djibre ameeleza kuwa Sekali ya Tanzania imeendelea kuwa rafiki na kutoa ushirikiano wakati wote ambao Taasisi hiyo imekuwa ikihitaji, hivyo kuifanya itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio.
Kwa upande wake Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amempongeza na kumshuruku Djibrine kwa uongozi wake mahiri katika kipindi chote alichoiongoza PAPU hasa katika kusimamia kwa mafanikio programu mbalimbali za Umoja huo na mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za Taasisi hiyo. Licha ya hayo Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amemwahidi Mhe. Djibrine kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itaendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake na hasa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo za kiutendaji na zakimazingira kadri zitakavyokuwa zikijitokeza.
Wazo la kuanzishwa kwa Umoja wa Posta wa Afrika (Pan African Postal Union – PAPU) lilitokana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliofanyika jijini Libreville, Gabon mwaka 1977 kwa lengo la kusimamia maendeleo ya Sekta ya Posta Afrika. Baadae, tarehe 18 Januari 1980 Umoja huo ulianzishwa rasmi na Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika uliofanyika jijini Arusha Tanzania tarehe 8 hadi 18 Januari 1980.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal Union - PAPU) Mhe. Younouss Djibrine akisaini kitabu cha wageni alipowasili alipowasili katika ofisi za Wizara jijini Dodoma. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.