Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza
ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile iliyopo
katika mikoa inayopakana na nchi jirani ili kuharakisha maendeleo ya maeneo
hayo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, alipowaongoza Wajumbe wa mkutano wa sita wa
tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi kutembelea miradi
mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mkoa wa Kigoma.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Eneo Maalum la Uwekezaji wa Kigoma (Kigoma Special
Economic Zone-KiSEZ); Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Bandari Kavu ya Katosho na
Bandari ya Kigoma pamoja na Kituo cha
Pamoja cha Kutoa huduma Mpakani (OSBP) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Manyovu
mkoani Kigoma.
Akiwa kwenye eneo Maalum la Uwekezaji, Prof.
Kabudi na Wajumbe wengine walijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye eneo
hilo na Kampuni ijulikanayo kama Next Gen Solar wa kuzalisha umeme wa jua wa
megawati tano ambao utaanza kusambazwa rasmi kwa wakazi wa Kigoma mwezi Aprili
2021. Upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa
mkoa huo kiuchumi.
Kadhalika Mhe. Prof. Kabudi na Wajumbe wengine
walipata fursa ya kutembelea kampuni ya Third Man Limited inayozalisha Asali
ijulikanayo kama Upendo (Upendo Honey) ambayo nayo imewekeza kwenye eneo hilo maalum
la KiSEZ. Katika maelezo yake kwa Mawaziri, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Alex
Scovic alisema kuwa Kampuni yake ambayo
inachakata asali inayozalishwa bila kutumia kemikali (organic) inanunua asali
hiyo kutoka kwa wafugaji wa nyuki zaidi ya 3,000 waliopo Kigoma na mikoa jirani
kama Tabora, Katavi, na Rukwa na baadaye kuiuza asali hiyo nje nchi hususan nchini
Marekani.
“Kampuni yetu ni ya kwanza kuwekeza kwenye eneo
hili. Tunazalisha Asali safi isiyo na kemikali ambayo ina soko kubwa nje ya
nchi hususan nchini Marekani. Biadhaa zetu tunazitangaza kuwa zimetoka Tanzania”
alisema.
Pia alijulisha kuwa, Kampuni yake imeajiri
zaidi ya vijana 60 wa kitanzania na kwamba mbali na kuchakata asali, kampuni hiyo
inazalisha nta ambayo huuzwa nchini Ujerumani ambao huitumia kwa ajili ya kutengeneza
vipodozi. Kampuni ya upendo huzalisha zaidi
ya tani 4,000 za asali kwa mwaka.
Katika ziara yao kwenye eneo la Bandari
Kavu la Kitosho, Mawaziri na Viongozi wengine walijulishwa kuwa eneo hilo
limeanzishwa maalum kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo
na bidhaa mbalimbali zinazokwenda Burundi kutokea Bandari za Tanzania. Tayari
eneo hilo limepata mzabuni atakayeanza ujenzi mwaka huu. Pia Mawaziri hao walitembelea Bandari ya Kigoma na
kupata fursa ya kujionea meli kongwe na ya kihistoria ya MV Liemba ambayo ina
miaka 108 tangu itengenezwe, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zote
zitaanza kufanyiwa ukarabati ili kuziwezesha kuendelea kutoa huduma kwa
wananchi wa Kigoma na kutoka nchi jirani.
Wakiendelea na ziara ujumbe huo ulitembelea
Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo ulipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROAD
wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma kuwa, mradi huo unalenga kupanua na
kukarabati maeneo mbalimbali ya Uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa
barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo awali ilikuwa na urefu wa mita 1800 na
sasa mita 1,300 zitaongezwa ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Pia mradi unalenga kujenga jengo la abiria,
maegesho ya ndege, usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa
jengo la kuongozea ndege, maegesho ya magari pamoja na uzio wa usalama.
Mhe. Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro walihitimisha ziara yao kwa
kutembelea eneo kitakapojengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP)
cha Manyovu na Mugina kwa upande wa Burundi. Wakiwa Manyovu waliweza kutembelea
maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa kwa upande wa Tanzania na upande wa
Burundi pamoja na kupokea taarifa ya mradi huo ambapo walijulishwa kwamba tayari usanifu wa ujenzi
wa kituo hicho cha Manyovu ambacho kitakuwa cha aina yake umeanza na
utakamilishwa mwishoni mwa mwezi Machi 2021.
Akitoa hotuba kuhitimisha ziara kwenye miradi
hiyo, Prof. Kabudi alisema Tanzania inawekeza kwenye miradi hiyo ili
kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi mbalimbalii
inazopakana nazo ikiwemo Burundi. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shingiro
alipongeza jitihada hizo za Tanzania na kuahidi kutumia fursa za miradi hiyo
ambayo mingi inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.