Na mwandishi wetu, Arusha
Baraza la
Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la
Jumuiya ya Afrika Mashariki lakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara
na kuimarisha biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo.
Awali akifungua
mkutano Jijini Arusha Ijumaa, Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango,
Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa mkutano huo ni
muhimu kwani utawawezesha mawaziri kupitia na kujadili miongozo ambayo
itasaidia kuboresha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo kuondoa
vikwazo visivyo vya kibiashara.
Aidha, Mhandisi
Mlote ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kanuni na sheria ya Afrika Mashariki,
vikwazo visivyo vya kibiasha baina ya nchi na nchi vimekuwa vikizuia ukuaji wa
biashara hivyo ni muhimu kupitia mkutano wa baraza la mawaziri kuangalia namna
ya kuviondoa ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndani ya jumuiya.
Nae Waziri wa
Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo amesema
kuwa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana mambo mengi ya
msingi ikiwemo kuendelea kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi.
“Tumezungumza
pia kuhusu ushiriki wetu katika kufanya biashara na Uingereza kwa kuzingatia
kuwa Uingereza siyo sehemu Jumuiya ya Ulaya, lakini pia tumezungumzia suala la
EAC kujiunga na jumuiya ya biashara ya Afrika ambayo sisi Tanzania tupo katika
hatua kadhaa na kuona kuwa na sisi tunajiunga na jumuiya hiyo mwaka huu,”
Amesema Prof. Mkumbo
Kwa upande wake,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amesema
kuwa mawaziri wamekubaliana kutoa msukumo wa biashara katika jumuiya ya afrika mashariki
lizingatiwe na kupea kipaombele na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara
katika nchi mbalimbali.
“Pamoja na mambo
mengine, pi tumekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru (Non-tarrif
barriers) viondolewe kwani vimekuwa vikikwamisha biashara bila sababu za
msingi, na kuangalia jinsi ya kuwekeza kwenye eneo la uwekezaji ndani ya
jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvutia
wawekezaji” amesema Mhe. Mwambe
Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na maamuzi ya ripoti ya mawaziri wa fedha, ripoti ya kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati ya uwekezaji.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya Mhe. Betty Maina, Waziri wa Viwanda na Biashara, - Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.
Wengine ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Mhe. Beata Habyarimana, Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Mhe. Grace Choda, pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Balozi Jeremie Banigwaninzigo.
Mkutano huu ni maelekezo ya Wakuu wa Nchi na
Serikali katika ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliyoifanya nchini Kenya tarehe 04 hadi 05 Mei, 2021.
Waziri wa
Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo akifafanua
jambo katika mkutano wa Baraza la kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda,
Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki leo jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji)
Mhe. Geofrey Mwambe. Kulia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda -
Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban. Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Waziri wa Viwanda
na Biashara kutoka Kenya, Mhe. Betty Maina akiwasilisha hoja kwenye mkutano wa
Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji
(SCTIFI). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi
Steven Mlote
Ujumbe wa Uganda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) Ujumbe wa Rwanda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) Ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.