Friday, June 25, 2021

MAWAZIRI WA EAC WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI, MAWASILIANO NA HALI YA HEWA


Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia Sekta ya Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa leo tarehe 25 Juni 2021 kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya sekta ya uchukuzi, mawasiliano na hali ya hewa. Makubaliano haya yamefikiwa katika Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa (TCM) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Lengo la Mkutano huo wa 17 wa TCM pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kupitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na kupitia na kujadili utekelezaji wa sera, mikakati, miradi na program mbalimbali katika sekta ya Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa. 

Miongoni mwa maeneo ambayo Mawaziri hao wamekubaliana kushirikiana ni pamoja na mapendekezo ya Taasisi ya Afrika Mashariki kuratibu programu za maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano; utekelezaji wa miradi na programu katika sekta ndogo ya barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa njia ya maji, hali ya hewa na mawasiliano.

Akizungumza baada ya Mkutano huo, Mwenyekiti Mhe. Wavinya Ndeti ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Miundombinu wa nchini Kenya amesema kuwa makubaliano muhimu yaliyofikiwa yatafungua zaidi fursa zinazotokana na sekta ya uchukuzi na usafirishaji kupitia anga, bararaba, reli na maji. Aliongezea kusema hatua hii itachangia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya maisha ya watu katika Jumuiya. 

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo Mhe. Mhandisi Dkt. Leonard Madaraka Chamulio (Mb) Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameeleza “tumekubaliana katika masuala yote tuliyojadiliana na hivyo tumeyapeleka katika Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, vilevile tumejadili na kupeleka mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya kuhusu uunganishaji wa huduma katika anga la Afrika Mashariki”.

Kwa upande wa Tanzania ushirikiano huu katika sekta ya anga unatarajiwa kuongeza mapato ya nchi kwa kuwa huduma za uongozaji ndege zitatozwa kutokana na ukubwa, uzito na muda utakaotumiwa na ndege kupita katika Anga la Tanzania.

Mkutano huo wa Mawaziri ambao awali ulitanguliwa na mikutano ya Wataalam na Makatibu Wakuu iliyofanyika kwa nyakati tofauti kuanzia ya tarehe 21 hadi 24 Juni 2021 jijini Dar, licha ya kupitia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri wa Jumuiya wamepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao na Makatibu Wakuu ikiwemo, mapendekezo kuhusu Taasisi ya Afrika Mashariki kuratibu programu za maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Dkt. Leonard Madaraka Chamulio akichangia jambo kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akifuatilia Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Afisa Uchumi Bi. Edna Chuku kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea.

Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote akifafanua jambo kweye Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam

Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Masharikia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini taaraifa ya Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano, na Hali ya Hewa uliofanyika katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam

Wajumbe wakifuatilia majadala uliokuwa ukiendelea katika Mkutano.
 

Mkutano ukiendelea


                                          Mkutano ukiendelea

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.