Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda, na Wakulima Tanzania (TCCIA) Bw. Paul Koyi pamoja na Mratibu wa Kanda wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima Afrika Mashariki (EACCIA) Bw. Charles Kahuthu walipomtembelea ofisini kwake tarehe 16 Juni 2021 Jijini Dodoma.
Ujumbe huo unaosimamia masuala
mbalimbali ya sekta binafsi ulikutana na Mhe. Balozi Mulamula kwa lengo la
kuwasilisha serikalini kusudi la sekta hiyo kuipendekeza Tanzania kuwa mwenyeji
wa Kongamano la Biashara na Viwanda linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 30
Agosti hadi 3 Septemba 2021 katika kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Lengo la kongamano hili ni
kuziunganisha sekta binafsi ili zipate uzoefu zaidi katika masuala ya viwanda
na biashara. Pia kuviandaa vyama vya biashara, viwanda na kilimo vya kanda kuwa
tayari kwa ushindani wakati huu ambapo mataifa ya Afrika yanajiweka tayari
kuingia katika soko huru la biashara la Afrika (CFTA).
Aidha, Rais wa TCCIA Bw. Koyi
alieleza kuwa kongamano hilo
litaambatana na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na sekta
binafsi hivyo, itakuwa ni fursa nzuri kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kushiriki
katika kongamano hilo ili kujifunza masuala ya biashara na uwekezaji.
Naye mratibu wa kanda wa
EACCIA, Bw. Charles Kahuthu alifafanua malengo madhubuti ya chama hicho katika
kuhakikisha kongamano hilo linakuwa tofauti na makongamano mengine yaliyokwishafanyika
ni pamoja na kuhakikisha kinaongeza ushirikiano na kanda nyingine ndani ya
Afrika ili kuweza kufungua fursa zaidi kwa wananchi wake.
“Sisi waratibu wa sekta binafsi
tumepanga Kongamano hili liwakutanishe wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika
Mashariki, nchi za Maziwa makuu, na nchi nyingine ndani ya Afrika” alisema Bw.
Kahuthu
Akiongea na ujumbe huu Mhe. Balozi Mulamula ameihakikishia sekta binafsi juu ya utayari wa serikali katika
kuhakikisha inafanikisha jitihada hizi zenye lengo la kuinua uchumi na kwamba
itakuwa bega kwa bega kutoa ushirikiano wakati wa maandalizi na wakati wa
kongamano.
Vilevile, ametoa wito kwa
TCCIA kuiandaa sekta binafsi kushiriki kikamilifu kuzinadi fursa mbalimbali
katika kongamano hilo. Pia akaongeza kuwa kongamano litasaidia katika kupeana
uzoefu wa kukuza mitaji na masoko ya biashara nje ya mipaka ya Tanzania sambamba
na kuvutia uwekezaji.
Kadhalika, ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kutumia fursa mbalimbali zitakazopatikana kupitia ugeni huo utakaowasili nchini.
Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Afrika Mashariki (EACCIA) chenye makao yake makuu nchini Kenya ni mdau muhimu katika kusimamia masuala ya sekta binafsi ndani ya jumuiya na pia kimekuwa kikiainisha vipaumbele mbalimbali vya sekta binafsi ndani ya jumuiya kwa kushirikiana na vyama vya kitaifa vinavyosimamia sekta hiyo.
Mazungumzo yakiendelea. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.