Na Mwandishi Wetu,
Katika kusheherekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 60 ya uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wake nchini Marekani imefanya Kongamano kwa njia ya Mtandao kuhusu biashara ya bidhaa za Kilimo za Tanzania.
Mkutano huo umeandaliwa kwa
kushirikiana na Taasisi za Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT),
Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Sister Cities International na Thunderbird
School of Global Management. Lengo la Kongamano hilo lilikua ni kuimarisha
mauzo ya bidhaa za kilimo za Tanzania nchini Marekani.
Kongamano hilo lilishirikisha wajumbe
kutoka Serikali za Tanzania na Marekani, Wafanyabishara na wadau wa kilimo wa
nchi hizo mbili na Taasisi za Fedha, ambapo Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf
Mkenda (Mb), ameshiriki kwenye Kongamano hilo, kadhalika, Meya wa Jiji la Helena-West, Arkansas,
Mstahiki Kevin Smith naye pia ameshiriki.
Wakati wa Kongamano hilo, fursa
mbalimbali za biashara ya mazao kati ya Tanzania na Marekani zilijadiliwa.
Mazao hayo ni pamoja na maparachichi, ufuta, samaki, asali, kokoa, mchele, mvinyo,
pareto, na mazao ya bahari.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, pamoja
na kueleza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya
kilimo na kuongeza mauzo ya nje, Mhe. Waziri Prof. Mkenda ameeleza pia
changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo pamoja na fursa za uwekezaji pamoja na
kuwasihi wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Meya
Kevin Smith ameeleza kwamba Jiji lake la Helena-West linalima mchele kwa
wingi na lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika biashara ya zao hilo.
Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Balozi
wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Dkt. Elsie Sia Kanza, ameeleza kuwa Kongamano
hilo ni mwanzo wa makongamano mengine mengi ya namna hiyo, kwa sababu Ubalozi
umejizatiti kuimarisha mauzo ya bidhaa mbalimbali za Tanzania nchini Marekani,
hasa bidhaa za kilimo. Pamoja na mambo mengine, Balozi Kanza ameahidi Ubalozi
utaendelea kushirikiana na mwekezaji au mfanyabiashara yeyote mwenye lengo la
kuwekeza Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.