Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan imejipambanua kuwa imedhamiria kuboresha mazingira ili kutoa
fursa kwa wadau kushiriki katika sekta mbalimbali, iwe siasa, biashara,
uwekezaji au masuala ya usawa wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata
Mulamula (Mb) alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark
anayehusika na Masuala ya Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon jijini Dar Es
Salaam tarehe 28 Februari 2022.
Balozi Mulamula
alieleza kuwa tokea Rais Samia aingie madarakani Serikali yake imechukua hatua
mbalimbali za kuboreha mazingira ya biashara na uwekezaji, kutoa uhuru zaidi wa
kisiasa, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha
ushirikiano na nchi za nje na mashirika ya kimataifa, kuboresha miundombinu na
kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19.
Balozi Mulamula
alieleza kuwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Denmark umetimiza
miaka 60 sasa, na katika kipindi hicho, nchi hizo mbili zimeshirikiana katika maeneo
mengi ikiwemo Tanzania kufaidika na misaada ya Denmark katika sekta tofauti kama
vile; huduma za afya, elimu, mabadiliko ya mifumo ya kodi, nishati, kilimo, athari
za mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.
Mhe. Waziri
alimuhakikishia Bi. Machon kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Denmark na
kusisitiza umuhimu wa nchi hiyo kuendelea kuisaidia Tanzania hususan, kwa
kuunga mkono jitihada za kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi wa Denmark kuja
kuwekeza nchini ili pamoja na mambo mengine uwekezaji huo uweze kutoa ajira kwa
vijana ambao idadi yao kwa nchi za Afrika ni kubwa.
Kwa upande wake, Bi. Machon alielezea utayari wa Denmark kuendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo tofauti yakiwemo ya demokrasia, nishati na mabadiliko ya tabianchi. Alisema nchi hiyo kila mwaka inatenga asilimia 1 ya pato lake kwa ajili ya misaada ya maendeleo kwa nchi marafiki ikiwemo Tanzania.
Ujumbe aliongozana nao Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Denmark anayehusika na Sera na Maendeleo, Bi. Lotte Machon ukinukuu dondoo muhimu za mazungumzo. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akitoa maelezo ya zawadi aliyomkabidhi Katibu Mkuu wa Denmark. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.