Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) zimeishukuru Tanzania kwa kujitolea kuwa Mwenyeji wa Kituo cha Kikanda
cha Kupambana na Ugaidi ambacho kimezinduliwa rasmi tarehe 28 Februari 2022
jijini Dar Es Salaam.
Kituo hicho kimefunguliwa na Waziri wa Kazi, Ajira,
Tija, na Ukuzaji wa Ujuzi wa Botswana, Mhe. Machana Ronald Shamukuni,
kwa niaba ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia
ni Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mhe. Maledi Pandor.
Katika hotuba yake, Mhe. Shamukuni alisema kuwa
kujitolea kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kituo hicho ni kudhihirisha namna nchi
hiyo wakati wote, tokea enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere imekuwa
na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa suala la usalama katika kanda linapewa
kipaumbele.
Alibainisha kuwa kituo hicho ni cha kwanza na cha
aina yake katika Jumuiya za Kikanda barani Afrika. Hivyo, kitakuwa muhimu
katika kuratibu masuala ya upatikanaji wa habari za kitelejensia, kubadilishana
uzoefu na kutoa ushauri wa namna ya kuandaa Sera na programu za kukabiliana na
kuzuia ugaidi baina ya nchi wanachama wa SADC.
Mhe. Shamukuni alihitimisha hotuba yake kwa kueleza
kuwa wakati ufunguzi wa kituo hicho unafanyika, nchi za SADC zimeshatuma tayari
kikosi cha kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyotokea katika jimbo la Cabo
Delgado nchini Msumbiji. Amekitaja kitendo cha kutuma kikosi hicho ni ishara ya
dhati ya nchi wanachama ya kuhakikisha kuwa zinakabiliana na vitendo vya ugaidi
na kuvikomesha kabisa katika kanda ya SADC.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Mhe. Stergomena Tax (Mb) alieleza kuwa matishio ya kigaidi ni
suala linalohitaji kushughulikiwa kwa nguvu zote, na kwa ushirikiano bila ya
kupepesa macho, na kuwasihi wanachama wa SADC kuikabili changamoto ya ugaidi kikamilifu.
Alieleza kuwa ugaidi si vita ya kawaida, ambapo
adui anaonekana kwa uwazi kwa sababu baadhi ya wafuasi wa vikundi vya ugaidi ni
sehemu ya tunaoishi nao na vitendo vyao vimesababisha madhara ya kiuchumu,
kijamii na kiusalama kwa raia wasio na hatia.
Alimalizia kwa kuainisha kuwa, kwa mujibu wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuanzia mwaka 2007 hadi 2016,
Bara la Afrika limepoteza Dola za Marekani bilioni 119 kwa ajili ya kukabiliana
na vitendo vya ugaidi, hivyo, nchi za Afrika endapo zitashirikiana ipasavyo kukomesha
vitendo hivyo, fedha nyingi zitaokolewa na kutumika kwa ajili ya mipango ya
kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Hafla ya ufunguzi wa kituo hicho ilihitimishwa kwa uwekaji
saini wa Mkataba wa Uenyeji ambao kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula na
kwa upande wa SADC ulisainiwa na Katibu Mtendaji, Mhe. Elias Magosi. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.