Balozi
Possi Afanya Ziara ya Kikazi Jamhuri Czech
Balozi wa Tanzania katika
Jamhuri ya Czech mwenye makazi yake Berlin, Ujerumani, Dkt. Abdallah Possi amefanya
ziara ya kikazi katika nchi ya Jamhuri ya Czech na kufanya mazungumzo na Naibu
Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Miloslav Stašek; Naibu Waziri wa Afya, Mhe.
Jakub Dvořáček na Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Prof. Jaroslav Miller tarehe 17
Machi 2022.
Wakati wa mazungumzo na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Possi aliwasilisha ombi ili Watanzania waweze
kunufaika na Mpango wa Nafasi za Ufadhili wa Masomo unaoratibiwa na Wizara
hiyo. Kwa sasa, nchi za Africa zinazonufaika na mpango huo ni Zambia na
Ethiopia. Mhe, Naibu Waziri aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo. Aidha, Mhe. Stašek
aliwasilisha mualiko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kufanya ziara ya kikazi Jamhuri ya Czech.
Katika mazungumzo yake
na Naibu Waziri wa Afya, Balozi Possi aliomba Serikali ya nchi hiyo kuangalia
uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta ya Afya, hususan
katika magonjwa ya moyo na figo. Serikali ya Jamhuri ya Czech imeahidi
kulifanyia kazi ombi hilo na kuahidi pia kuwa ipo tayari kuisaidia Tanzania
dozi za chanjo ya UVIKO-19.
Kwa upande wa
mazungumzo na Naibu Waziri wa Elimu, wawili hao walijadili kuhusu ushirikiano
wa Vyuo Vikuu, na namna ambavyo wanafunzi wa Tanzania waliokatiza masomo nchini
Ukraine wanaweza kurahisishiwa mchakato wa kuhamisha alama na kumalizia masomo
yao katika vyuo vikuu vya Czech. Prof.
Miller alimweleza Balozi Dkt. Possi wataanza na utaratibu wa awali wa
kuvitaarifu vyuo vikuu vya Czech na kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa Tanzania,
huku taratibu nyingine za kiufundi zikifuata.
Mhe. Miller aliahidi pia
kuwa mamlaka husika zitaweka tangazo katika tovuti ya “Study in Czech Republic”
ili kuwahamasisha wanafunzi wa Tanzania waliokuwa
Ukraine kuomba kujiunga na vyuo vikuu Jamhuri ya Czech.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.