Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Serikali ya Jamhuri ya Czech Balozi Miloslav Machalek katika mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Mjumbe huyo maalum wa Serikali ya Czech Balozi Machalek amewasilisha andiko la Serikali ya nchi hiyo la kutaka kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya usimamizi wa maji, kilimo, afya, ICT na biashara.
Akizungumza katika kikao hicho Balozi Sokoine ameongelea kufurahishwa na wazo la kuihusisha Tanzania katika mradi huo ambao alisema kuwa utaimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Czech.
Balozi Machalek amesema andiko aliloliwaasilisha katika kikao hiko ni mradi wa maendeleo ambao nchi yake unakusudia kuutekeleza katika nchi tano za Afrika za Tanzania, Tunisia, Kenya, Ghana na Ivory Coast.
Balozi Machalek aliambatana na Balozi wa Jamhuri ya Czech nchini Tanzania mwenye makazi yake nchini Kenya Mhe. Martin Klepetko ambaye pia alitumia fursa hiyo kuzungumza na Balzoi Sokoine katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Czech.
Naye Balozi wa Jamhuri ya Czech ameelezea nia ya Serikali ya Czech kushirikiana zaidi na Tanzania kupitia Nyanja za biashara na uwekezaji ili kukuza ushusiano na ushirikiano kwa faida ya pande zote mbili na kuongeza kuwa ni matumaini yake kuwa uhusiano mzuri ulipo baina ya nchi hizo utaendelea kuimarika.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.