Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 06 Mei, 2022.
Akiongelea mkutano huo Mhe. Waziri amesema Mkutano huo umejadili masuala ya madhara yaliyotokana na mafuriko yaliyozikumba baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo na Mkataba Cotnou ambao unaongelea ushirikiano kati ya nchi za Afrika, Pasifiki na Carebean na Jumuiya ya SADC ili kuhakikisha ushirikiano baina ya nchi unaimarika.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mulamula alitoa salamu za pole kwa nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Mauritius na Malawi kufuatia mafuriko makubwa yaliyozikumba nchi hizo na kusababisha vifo vya wananchi wake, hasara ya mali na miundombinu katika nchi hizo.
‘‘Kupitia Mkutano huu nitoe pole nyingi kwa wananchi wa nchi wanachama wenzetu kutokana na mafuriko yaliyotokea katika nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Madagascar na Malawi, mafuriko ambayo yameziletea nchi hizo madhara makubwa kama vile vifo vya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu,’’ alisema Balozi Mulamula.
Katika mkutano huo nchi wanachama kwa ujumla wao waliangalia madhara yaliyotokana na mafuriko hayo na namna ambavyo jumuiya hiyo inaweza kuzisaidia nchi zilizoathirika.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nansy Tembo uliridhia utoaji wa fedha kutoka katika Mfuko wa Maafa wa Jumuiya ya SADC kwa ajili ya kusaidia nchi hizo zilizoathiriwa na mafuriko hayo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.