Friday, May 6, 2022

TANZANIA YASHIRIKI MAONESHO YA KILIMO YA MACFRUT 2022 ITALIA

Katika jitihada za kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo, Tanzania kwa mara ya kwanza imeshiriki katika maonesho ya kimataifa ya kilimo yanayojulikana kama MACFRUT FIERA yanayoendelea mjini Rimini, nchini Italia.

Maonesho hayo yanawakutanisha wazalishaji, wanunuzi na wauzaji wa bidhaa za kilimo cha mbogamboga na matunda, ufugaji wa kuku na mashine za kisasa zinazotumika katika kilimo. 

Akifungua maonesho hayo, Waziri wa Kilimo wa Italia, Mhe. Stefano Patuanelli, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji na usalama wa chakula. 

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo umevutia ushiriki wa sekta binafsi katika maonesho hayo ambayo tunda la mwaka huu ni parachichi. 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, aliwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya kilimo na sekta nyinginezo.

“Nawahakikishia kuwa Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza kero zilizokuwa hapo awali na kwamba, Watanzania wapo tayari kuwapokea,” alisema Balozi Kombo. 

Maonesho ya MACFRUT hufanyika kila mwaka. Awamu inayofuata ya maonesho (MACFRUT FIERA 2023) itafanyika mwezi Mei, 2023 katika mji wa Rimini. 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na washiriki kutoka Angola waliotembelea banda la Tanzania katika maonesho ya MACFRUT

Maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Italia wakizungumza na baadhi ya washiriki waliotembelea banda la Tanzania katika maonesho ya a MACFRUT 

Washiriki kutoka Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja naBalozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo kwenye maonesho ya MACFRUT katika mji wa Rimini, Italia

Naibu Waziri Mkuu wa Uganda na mgeni rasmi katika kongamano maalum kwa ajili ya Afrika, Mhe. Rebecca Kadaga (katikati mwenye barakoa) akiungana na viongozi wengine kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa maonesho hayo uliofanyika tarehe 4 Mei 2022


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.