Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma na
wadau mbalimbali hapa nchini kuhusu fursa zitokananzo na Eneo Huru la Biashara Barani
Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ili kuwawezesha
kuzichangamkia kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe
29 Mei 2022 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Mbarouk
Nassor Mbarouk wakati akifungua rasmi Warsha ya Kueleimisha na Kujenga Uwezo
kwa Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Mkataba
ulioanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika.
Mhe. Balozi Mbarouk amesema
kuwa, watanzania wana kila sababu ya kuchangamkia fursa zinazotokana na Mkataba
wa AfCFTA na kunufaika nazo kwa kuwa Tanzania ni mwanachama kamili wa mkataba
huo baada ya Bunge kuuridhia mnamo mwezi Januari 2022. Fursa hizo ambazo ni
pamoja na Biashara, Ajira, Uwekezaji, Teknolojia zitainufaisha nchi kwa kukuza
pato la Taifa kutokana na eneo kubwa la soko, kukuza viwanda, ongezeko la
biashara ndani ya Afrika na kuongezeka uzalishaji na mnyororo wa thamani.
“Ili kuwawezesha wadau
kutambua na kutumia fursa za AfCFTA, Serikali imejipanga kuwa na mkakati
endelevu wa kutoa elimu kwa umma. Tayari Serikali imeanza kutoa elimu na
kujenga uwezo kwa wadau kwa makundi. Tayari Warsha za aina hii zimefanyika
Zanzibar, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza na zimehusisha Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi, Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi” amesema Mhe. Mbarouk.
Ameongeza kusema kuwa, AfCFTA
ni muhimu kwa Tanzania katika kupanua wigo wa soko la bidhaa na huduma nje ya
soko la EAC na SADC na kwamba Wizara inatumia fursa ya AfCFTA kutekeleza
mikakati ya Diplomasia ya Uchumi ya kuvutia wawekezaji nchini ilikuzalisha na kuuza kwenye soko la
AfCFTA.
Pia alitumia fursa hiyo
kuwaomba Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Mabalozi kwenye suala hilo na kushirikiana
na Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wadau ili Tanzania itumie ipasavyo fursa
zitokanazo na ushiriki wake katika AfCFTA.
“Nina imani kuwa kupitia
warsha hii, kila mmoja wetu atakuwa amepata elimu ya kutosha kuhusu mkataba wa
AfCTA pamoja na fursa zake na mtakuwa mabalozi wazuri kwenye suala hili katika
kushirikiana na Serikali” alisisitiza Balozi Mbarouk.
Akiwasilisha mada kuhusu
Mkataba wa AfCFTA, Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za
Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Bw. Bernard Haule amesema nchi 54 za
Afrika zimesaini Mkataba huo na tayari nchi 43 ikiwemo Tanzania zimeuridhia. Amesema malengo ya kuanzishwa mkataba huo ni
pamoja na kutengeneza soko moja la uhakika la kuhimili vishindo vya dunia;
kujenga na kukuza uzalishaji na uwezo wa uchumi wa viwanda barani Afrika na kuweka msingi utakaowezesha kuwa na umoja
wa forodha wa Afrika.
Kwa upande wake, Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,
Mhe.Vincent Mbogo ameipongeza na kuishukuru Wizara kwa kundelea kutoa elimu na
kushauri jitihada zaidi zitumike ili kuwafikia wananchi wa mijini na vijijini. Pia
amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwa na takwimu sahihi za mahitaji ya soko na
zile za uzalishaji ili kuwe na uwiano na mwendelezo kwenye ufanyaji biashara. Vilevile
elimu ya uzalishaji wa bidhaa bora na zenye viwango itolewe ili kukidhi matakwa
ya Soko hilo.
“Naipongeza Wizara kwa hatua
hii. Hata hivyo bado mna kazi kubwa ya kuwafikia watu wa mijini na vijijini ili
kuwaeleimisha kuhusu fursa zitokanazo na soko hili muhimu. Tumieni njia
mbalimbali kutoa elimu hii ikiwemo vyombo vya habari kama radio, televisheni na
mitandao ya kijamii ili elimu hii iwafikie wananchi kwa wingi” alisema Mhe.
Mbogo. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.