|
Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda na ujumbe wake wamekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya African Trust ya jijini Gaborone Bw. Monametsi Sokwe na kusikiliza maoni na mtazamo wake juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu yanavyokwenda nchini humo.
Bw. Sokwe ameshukuru kukutana na SEOM na kusema kuwa vyama vingi ni vichanga na havina nguvu za kifedha kuendesha shughuli zao za kisiasa hasa za kampeni wakati huu wa uchaguzi.
Mhe. Pinda amemuomba Bw. Sokwe na washirika wake kuhakikisha wanaongeza na kuwashirikisha kwa wingi wanawake na vijana katika shughuli za siasa kwani kufanya hivyo ndivyo kunachochea ukuaji wa demokrasia nchini humo.
Katika tukio jingine Mhe. Pinda na ujumbe wake mazungumzo kwa njia ya mtandao na Kiongozi wa Chama Kipya cha Siasa cha Botswana Republican Party (BRP) Bw. Biggie Butale ambacho kimesimamisha wagombea 10 katika nafasi ya viti vya Bunge la nchi hiyo.
Mhe. Pinda alieleza dhamira ya ujumbe wake kuzungumza na kiongozi huyo kuwa ni kutaka kusikia maoni na mawazo yake kuhusu namna kampeni za vyama vya siasa zinavyoendeshwa na kama mazingira ni mazuri na yanaridhisha kwa nyakati husika.
Bw. Biggie alielezea kuridhishwa kwake na namna shughuli za kuelekea uchaguzi mkuu zinavyoendeshwa na kwamba mazingira yamekuwa salama ila alielezea kutokuridhishwa kwake na wazo la kutoa fedha za uchaguzi kwa vyama vya siasa baada ya uchaguzi na kuongeza kuwa hatua hiyo haitoi nafasi kwa vyama vya siasa kuwa sawa na hivyo kuwapa manufaa vyama vikongwe na vikubwa na kuviacha vyama vichanga njiani.
Tarehe 30 Oktoba, 2024 Wananchi wa Botswana watapiga kura katika Uchaguzi mkuu kuchagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambpo Viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa.
SEOM imepeleka waangalizi wake wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.