Wednesday, October 23, 2024

BALOZI SHELUKINDO AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA BUNGE LA MAREKANI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani na ujumbe wao wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, leo tarehe 23 Oktoba 2024, amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Bunge la Marekani wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. 

Kupitia mazungumzo hayo wamejadili masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, utalii, demokrasia na utawala bora na ulinzi na usalama. 

Balozi Shelukindo akizungumza na ujumbe huo ulioongozwa na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani amewaeleza kuwa hali ya kisiasa nchini ni salama na tulivu. Katibu Mkuu Balozi Shelukindo alisisitiza kuwa hali hiyo inachagizwa na juhudi zinazofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Falsafa ya R4, ambazo ni Maridhiano, Mageuzi, Ustahimilivu na Kujenga upya.

Kwa upande wake Bi. Heather Flynn ameeleza kuridhishwa kwake na mageuzi mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo ameeleza kuwa ni muhimu katika ustawi wa siasa, jamii na uchumi wa Taifa.

Ujumbe wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Marekani ipo nchini kwa ziara ya kikazi, ambapo watakutana na kufanya mazungumzo na watendaji na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Bi. Heather Flynn, Mtaalamu wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge (Senate) la Marekani na ujumbe wakifurahia jambo walipokuwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.