Wednesday, October 23, 2024

NAIBU WAZIRI CHUMI AFANYA MAZUNGUMZO NA WABUNGE WA BUNGE LA AFRIKA


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Afrika (PAP) katika Ofisi ya Wizara jijini Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2024.

Wabunge hao wa Bunge la Afrika wa Kamati ya Biashara, Forodha na Uhamiaji wapo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku nane (8) yenye lengo la kujionea hatua iliyopigwa na Tanzania katika utekelezaji wa muongozo wa awali wa kufanya Biashara (Guided Trade Initiatives - GTI) wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Akizungumza na wabunge hao naibu Waziri Chumi ameeleza Tanzania imekuwa ikifanya shughuli nyingi za kibiashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla kupitia AfCFTA ambapo Tanzania ilichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 8 za mfano katika utekelezaji wa awali wa kufanya biashara. Nchi nyingine ni Rwanda, Ghana, Egypt, Mauritius,Cameroon na Tunisia.

AfCFTA ni sehemu ya utekelezaji wa Agenda 2063 iliyosainiwa Rwanda mwaka 2018 na Wakuu wa Nchi na Serikali ya Afrika ikiwa na matarajio ya kuwa na mtangamano wa kikanda wenye amani na ustawi.
 Aidha, amefafanua kuwa uratibu wa wafanyabiashara unafanywa na taasisi za biashara mfano taasisi ya sekta binafsi Tanzania, Chama cha wafanya biashara wenye viwanda na wakulima, Chama cha wafanyabiashara wanawake Tanzania na nyingine ambazo zimekuwa zikiratibu na kuwaunganisha na Serikali katika kuwezesha shughuli za kibiashara na kujenga uelewa wa masuala mbalimbali kwa wafanyabishara.

“Elimu kwa umma bado inahitajika katika kujenga uelewa kwa wafanyabiashara ili waweze kutumia fursa za masoko na biashara zinazopatika barani Afrika, hivyo Tanzania inaendelea kujenga uwezo katika hilo ili kuongeza fursa za mazao ya kibishara na taratibu za kufanya biashara” alisema Mhe. Chumi.

Naye, Mkuu wa ujumbe huo wa Wabunge hao na Mbunge wa Kenya, Mhe. Prof. Margaret Kamar  ameeleza kuwa Bunge la Afrika hushirikiana katika utendaji wake na Mawaziri wa Mambo ya Nje barani Afrika katika kuhakikisha malengo na mipango mbalimbali yenye maslahi ya kikanda inafikiwa.

Pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa kufanikiwa kufanya maboresho na mageuzi ya kibiashara hususan katika kuhakikisha inakua na barabara nzuri inayowezesha shughuli za kibiashara baina yake na nchi jirani na bara la Afrika kwa ujumla.

“ Miongoni mwa mikoa tuliyotembelea kabla ya kuja huku Dododma ni mkoa wa Arusha, tumejionea dhahiri namna barabara zilivyoboreshwa na kutuwezesha kutembelea kwa urahisi kila
sehemu tuliyohitaji kutembelea” Mhe. Kamar alisema.

Pia alibainisha kuwa huo ni ushahidi tosha kwa nchi nyingine za Afrika kuona kuwa inawezekana kuiunganisha Afrika kibiashara endapo hatua madhubuti za kufanikisha hilo litapewa mkazo.

Vilevile ameeleza kuwa hatua hizo zilizopigwa zinaonesha kuwa Tanzania ina uwezo wa kupiga hatua zaidi kibiashara na kuzipita kanda nyingine kwakuwa ina nafasi na fursa za kutosha hususan kupitia uwingi wa rasilimali za kibiashara.

Msisitizo mwingine uliotolewa na Wabunge hao wa PAP ni pamoja na suala la uhuru wa watu kutembea baina ya nchi na nchi ambalo kwa upande mwingine linahitaji muongozo kwakuwa kwasasa bado halijielezi vizuri mipaka ya uhuru huo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi ameeleza kuwa Tanzania katika jitihada zake za kuwaunganisha Watanzania kibiashara barani Afrika, imefanikiwa kufanya yafuatayo; uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika, Ujenzi wa miundombinu hususan barabara, reli ya kisasa, kuimarisha shirika la ndege la Tanzania kwa kuongeza ndege ikiwemo ndege za mizigo zenye uwezo kusafiri popote duniani.

Pia Balozi Mbundi ameeleza kuwa GTI imewezesha usafirishaji wa bidhaa za biashara zilizoongezwa thamani ambapo kwa upande wa Tanzania ilianza kuuza bidhaa kama mkonge, kahawa, viungo na karanga.

Kadhalika, ujenzi wa Vituo vya Huduma za Pamoja Mipakani umewezesha kuondoa changamoto nyingi zilizokuwa kikwazo katika biashara na nchi nyingine. Vituo hivyo vimewezesha kuokoa muda kwa wasafirishaji wa bidhaa na wasafiri na kupunguza muda wa kupitisha bidhaa mipakani ambapo maboresho hayo yameenda sambamba na maboresho ya mizani ya kupima mizigo inayotoka bandarini na kuelekea katika nchi jirani.

Hata hivyo, Tanzania ipo katika hatua za mapitio za kutathimini bidhaa nyingine ambazo zitafaa kuingia katika utekelezaji wa Muongozo wa Awali wa kufanya Biashara ili kuona namna gani
inanufaika na soko la AfCFTA.

“Nchi zetu za Afrika zinazalisha bidhaa zinazofanana hivyo ni lazima tathimini yetu ifanyike kwa kina ili kupata bidhaa zenye upekee, tofauti na bidhaa za nchi nyingine na kuleta tija katika maendeleo ya biashara nchini’’ alisisitiza Balozi Mbundi.




Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) akizungumza na wabunge wa Bunge la Afrika walipomtembea ofisini kwake jijini Dodoma tarehe 22october 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akichangia mada wakati wa mazunguzo.


Naibu Waziri Mh. Cosato David Chumi akizungumza na sehemu ya wabunge waliokuja nchini kwa ziara ya siku nane.



Picha ya pamoja


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.