Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewashukuru
wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kupitisha kwa
kauli moja Azimio linalotaka pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuwasilisha taarifa kuhusu watu wenye ualibino.
Azimio hilo na ambalo liliandaliwa kwa pamoja kati
ya Wakilishi za Kudumu za Tanzania na Malawi katika Umoja wa Mataifa,
limepitishwa siku ya Jumanne baada ya majadiliano ya kina na jumuishi
yaliyowashilikisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Akiwasilisha Azimio hilo mbele ya wajumbe wa Kamati
hiyo ambayo inahusika na masuala ya Haki za Binadamu, Utamaduni na Maendeleo ya
Jamii, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako
Manongi amesema
“Azimio hilo linalenga katika kuitaka jumuiya ya
kimataifa kutambua na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili
watu wenye ualibino”
Akabainisha kwamba ni kwa kutambua changamoto hizo
zikiwano za kielimu, kiafya na kiuchumi pamoja na hatari zinazowakabili kwa
sababu tu ya kuwa na ualibino ndio maana Tanzania kwa kushirikiana na Malawi
ziliamua kuanda na hatimaye kuwaalika nchi wanachama si tu kulijadili na
kuboresha mapendekezo yaliyomo katika azimio hilo bali pia kuliunga mkono.
Balozi Tuvako Manongi akawaeleza wajumbe wa Kamati
ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, katika eneo la afya watu
wenye ualibino wanakabiliwa na tatizo kubwa la kansa ya ngozi kutoka na hali hiyo.
Tatizo alilosema linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kuwasaidia.
“Azimio hili linalenga katika kuelezea pengo
lililopo kuhusiana na changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino hususani katika
elimu, afya, na ajira . Matatizo yao na changamoto zao na kwa kuwa
yanaingiliana yanahitaji ushiriano kati yetu sisi sote na ufumbuzi wa muda
mrefu” akabinisha Balozi Manongi.
Na kuongeza kuwa hakuna matibabu au uponyaji kwa
watu wenye ualibino lakini kuna baadhi ya nchi chache ambazo zimeweza kubuni
sera za kijamii na za afya za kuwasaidia watu wenye ualibino. Na kwamba
ushirikiano kati ya nchi hizo chache ambazo zina sera nzuri za afya na zile
ambazo hazina uwezo mkubwa wa raslimali ni jambo ambalo Tanzania inapenda
kupitia azimio hilo kuona ukiimarishwa na kuwa shirikishi.
“Tunawashukuru wale wote ambao wameshirikia katika
majadiliano ya awali ya maandalizi ya Azimio hili kwa mchango wao wa mawazo
lakini pia kwa kuliunga mkono Azimio hili. Hapashaka Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa atawasilisha taarifa yake kama alivyoombwa kupitia Azimio hili.
Kwa mujibu wa Azimio hilo,Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa anatakiwa kuwasilisha Taarifa kuhusu watu wenye ualibino wakati wa
kipindi cha Baraza Kuu la 72 la Umoja wa Mataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni tatizo na changamoto
zinazowakabili watu wenye ualibino limekuwa likipewa uzito wa aina yake katika
Jumuiya ya Kimataifa.
Mwaka jana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
lilipitisha Azimio ambalo lilitamka kwamba Juni 13 ya kila mwaka inakuwa siku
ya Kimataifa ya watu wenye ualibino. Na mwezi Machi mwaka huu Baraza la Haki za
Binadamu liliteua mtaalamu wa kujitegemea kuhusu haki za binadamu za watu wenye
ualibino.
Azimio lililoandaliwa na Tanzania na Malawi ni
mwendelezo wa juhudi kutafuta namba bora na jumuishi za kuwasaidia na
kuwaendeleza watu wenye ualibino.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.