Friday, October 23, 2020

NCHI ZA AFRIKA ZAHIMIZWA KUSHIKAMANA ILI KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

Nchi za Afrika zimehimizwa kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi jambo litakaloliwezesha Bara hilo kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Mabalozi wa nchi za Afrika hapa Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed wakati Mabalozi hao walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ikiwa ni utaratibu wa kukutana na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.

Kiongozi huyo wa Mabalozi hapa nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro amesema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara hilo linaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara hilo kujitegemea.

"Njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa sisi kama waafrika tunaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara letu kujitegemea kwa umoja, mshikamano wetu wenyewe," Amesema Dkt. Mohamed

Nae Balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu amesema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.

"MKutano wa leo umetuwezesha sisi mabalozi wa Afrika tunaowakilisha nchi zetu hapa Tanzania kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo," Amesema Balozi Kazungu.   

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika,kulinda demokrasia na haki za binadamu lakini pia kutumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.  

"Waheshimiwa Mabaalozi napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania inaheshimu na imedhamiria kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za binadamu pamoja na kuhakikisha kuwa inatumia fedha zake za ndani katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa," Amesema Prof. Kabudi.  

Mkutano huo uliohudhuriwa Mabalozi 15 na wawakilishi wa Balozi 8 walitumia fursa hiyo kumuombea Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere kama Baba wa demokrasia Barani Afrika pamoja na kuuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Mabalozi waliohudhuria katika mkutano huo ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed, Balozi wa Msumbiji, Mhe. Patricio Clemente, Balozi wa Namibia, Mhe. Theresia Samaria, Balozi wa Somalia, Mhe. Mohammed Abdi, Balozi wa Morocco, Mhe. Abdelilah Benryane, Balozi wa Zambia, Mhe. Benson Chali.

Wengine ni Balozi wa Burundi, Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Kenya, Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Ethiopia, Mhe. Yonas Yosef Sanbe, Balozi wa Misri, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abdulwafa, Balozi wa Angola, Mhe. Sandro De Oliveira, Balozi wa Malawi, Mhe. Chembe Mnthali, Balozi wa Saharawi, Mhe. Mahayub Buyema, Balozi wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali, Charles Karamba pamoja na Balozi wa Algeria, Mhe. Ahmed Djelal.

Wawakilishi waliowakilisha Balozi nane ni Bw. Jaafar Nasir Abdalla kutoka Ubalozi wa Sudan, Mr. Sizwe Ernest Mayoli kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini, Balozi William Wani Ruben kutoka Ubalozi wa Sudani Kusini, Bibi. Bintu Bwala Ekikor kutoka Ubalozi wa Nigeria, Bw. Kamal Krista kutoka ubalozi wa Libya, Bw. Adjanga Bissa Benjamin kutoka ubalozi wa DRC, Bibi. Musekura Esezakutoka ubalozi wa Uganda pamoja na Bw. Chrispen Chibuwe kutoka Ubalozi wa Zimbabwe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mabalozi mbalimbali wa nchi za Afrika hapa nchini Tanzania leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwaonesha Mabalozi (hawapo pichani)  ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati mkutano ukiendelea



Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Mabalozi ukiendelea  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza mkutano



Wednesday, October 21, 2020

TROIKA YA SADC YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UCHAGUZI MKUU

Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama (TROIKA) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeridhishwa na mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28,2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo.

Akizungumza katika Mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema TROIKA imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu tangu awali mchakato wa uchaguzi hapa nchini na kwamba imeridhishwa na mazingira ya amani yaliyopo hali inayoruhusu uchaguzi huo kufanyika.  

"Leo katika mkutano wangu na TROKA ulifanyika kwa njia ya mtandao mwenyekiti wa TROIKA ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana Dkt. Lemogang Kwape ameoneshwa mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, 2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo," Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipate uhuru kwamba uchaguzi huu unagharamiwa kwa fedha ya walipa kodi maamuzi ambayo yamefanyika kwa kutambua kuwa demokrasia ndio jambo kubwa katika uhai,utashi na kielelezo cha Taifa ambalo ni huru kama ilivyo Tanzania.

Kuhusu waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Octoba 28, Prof Kabudi amesema TROIKA imefanya tathimini ya awali ya hali ya usalama na kisiasa na kwamba Tanzania inategemea kuwapokea waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na wale wa kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson.

Katika mazungumzo yao Prof. Kabudi amesema WFP imekuwa ni miongoni mwa mashirika ya Kimataifa ambayo yanaushirikiano mzuri na Tanzania ambapo kwa mwaka 2018 WFP imenunua tani 160,000 za nafaka na 2019 wamenunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 21 fedha ambazo zimesaidia wakulima wadogowadogo katika kuboresha kilimo.  

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson amesema wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano baina ya pande hizo mbili hususani kusaidia wakulima wadogowadogo nchini kuboresha kilimo,kuboresha mazingira ya lishe na kwamba shirika hilo lina mpango wa kuongeza msaada wanaoutoa kwa Tanzania. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akieleza jambo wakati mkutano wa TROIKA ukiendelea. Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao leo Jijini Dar es Salaam.  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akipokea nakala ya hati za utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi leo jijini Dar es Salaam



Monday, October 19, 2020

CHINA: TUHESHIMIANE, KUACHA KUINGILIA MASUALA YA NDANI YA NCHI NYINGINE

China imetoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa kwake na namna mchakato wa Uchaguzi mkuu unavyoendelea hapa nchini.

Kauli hiyo imetolea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kuongeza kuwa ni lazima Mataifa yote yaendeleze mahusiano mema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya Mataifa mengine.  

"Ni vyema Mataifa yote yakaendeleza mahusiano mema miongoni mwao na kuhakikisha kuwa hayaingilii masuala ya ndani kati ya Taifa moja na jingine," Amesema Balozi Wang Ke.  

Aidha Balozi Wang Ke ameongeza kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya Mataifa yote Tanzania ikiwemo na kueleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema  ushirikiano iliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara na kwamba Tanzania itaendelea pia kuheshimu mashirikiano na mataifa mengine.  

Aidha Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

"Serikali ya Tanzania kwa kweli inaishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati na tunakuahidi kwamba uhusiano wetu utaendelea kudumishwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili," amesema Balozi Ibuge.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo Jijini Dar es Salaam

Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge



Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke akimkabidhi kitabu kinachoelezea maendeleo ya China Katibu  Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge





Friday, October 16, 2020

BALOZI IBUGE AKUTANA, KUMUAGA BALOZI WA NIGERIA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amekutana na kumuaga Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada ambaye amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini.  

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Ibuge amemtakia maisha mema na kumsihi kuwa balozi mwema kwa Tanzania nchini Nigeria na kwingineko duniani.

Balozi Ibuge amesema kuwa Nigeria imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Tanzania hasa katika kuunga mkono jitihada za kuimarisha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta za usafirishaji, utalii, biashara na uwekezaji na usafirishaji

“Leo nimekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Gada ambae amemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini na anarudi Nigeria, na kwa hakika mazungumzo marefu na yamelenga urafiki baina ya nchi zetu mbili na watu wetu pamoja na ushirikiano uliopo wa kibiashara, kibenki lakini pia tumezungumzia namna ambavyo Nigeria inapiga hatua kama Tanzania inavyopiga hatua, na mfano mzuri ni kuwa Nigeria ilipojenga mji wake mkuu mpya (Abuja) walikuja Tanzania kuja kujifunza na kupata ramani ya Dodoma ambayo wamemaliza kuijenga na sisi sasa tunaendelea kuijenga Dodoma tangu tulipotangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 1973" Amesema Balozi, Brigedia Jenerali Ibuge  

Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amemhakikishia Balozi Gada, kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Nigeria utaendelea kuimarika ikiwa ni ishara ya kuwaenzi waasisi wa mataifa ya Tanzania Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Nigeria Nnamdi Azikiwe ambapo viongozi hawa walikuwa ni sehemu ya juhudi za kukomboa bara la Afrika na hata kusimi mwa Afrika. 

Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesisitiza kuwa Tanzania na Nigeria zitaendelea kushirikiana katika sekta ya uwekezaji na biashara kwa maslahi mapana ya mataifa yote mawili ambapo pia ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchini Nigeria kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta za benki na utalii. 

Kwa upande wake, Balozi Sherlock ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliyompatia wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri na imara tangu miaka ya 1962.

”Nimekuja kumuaga Katibu Mkuu kama ishara ya ushirikiano wetu kati ya Nigeria na Tanzania kwa kweli nashukuru sana kwa ushirikiano nilioupata wakati wa utumishi wangu hapa nchini, nikiwa hapa nimeona uchumi wa Tanzania ukikua kila wakati jambo ambalo ni zuri hapa kwetu Afrika, pia namshukuru Katibu Mkuu, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kwa kuuendeleza ushirikiano wetu kwa kweli naiona Tanzania kama nyumbani kwangu pia,"Amesema Balozi Gada.  

Nigeria itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania za kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo,” amesema Balozi Gada.

Tanzania na Nigeria zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu Serikali ya Nigeria ilipofungua ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 1962.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimkaribisha Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada alipokenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati alipokwenda kumuaga leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akimuelezea jambo Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakati alipokwenda kumuaga   


Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada  

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Dkt. Sahabi Isa Gada wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Nigeria hapa nchini 








Tuesday, October 13, 2020

Tanzania Kutumia Maonesho Makubwa ya Qatar Kutangaza Utalii


Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Fatma Rajab alikutana na Shirika la Qatar Travel Mart (QTM) linalojishughulisha kutangaza utalii wa ndani na nje ya Qatar pamoja na kuandaa Maonesho ya Utalii. Shirika hilo linajiandaa kufanya Maonesho Makubwa ya Utalii  yatakayofanyika tarehe 17-19 November 2021. Mataifa mengi ya kigeni ya Asia, Ulaya na Marekani yanatarajiwa kushiriki Maonesho hayo pamoja na ofisi za Kibalozi ziliopo Qatar.

 Maonesho hayo yatatoa fursa kwa nchi kutangaza Biashara, uwekezaji na Sanaa. Mhe. Balozi amewaahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu kwenye Maonesho hayo. Aidha kabla ya Maonesho hayo Ubalozi utaandaa Mkutano wa Mtandao Webinar Conference mwezi Desemba 2020 baina ya Shirika hilo la QTM na TTB na ZTC ili kuelezea vivutio vya Utalii vya Tanzania na kukaribisha watalii kutoka Qatar

 

Friday, October 9, 2020

TANZANIA,CHINA ZAKUBALIANA KUIMARISHA MAHUSIANO YA KIMKAKATI

 Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza mahusiano ya kimkakati baina yao ili kuwezesha uwepo wa ulingo sawa miongoni mwa mataifa katika kusimamia maslahi na maendeleo ya nchi husika katika jumuiya za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John kabudi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke na kusisitiza umuhimu wa Mataifa kuheshimiana na kutokubali kuingilia uhuru wa mambo ya ndani ya nchi kwa kisingizio cha haki za binadamu,demokrasia ama jambo lolote jingine.  

Ameongeza kuwa mazungumzo hayo ya kimkakati yalilenga pia kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa 55 tangu Tanzania na China zisaini mkataba wa urafiki ambao uliweka msingi wa mahusiano makubwa na ya dhati  katika nyanja za ulinzi na usalama,afya,kilimo, elimu na miundo mbinu ambapo mpaka sasa China ni Taifa linaloongoza hapa nchini kwa uwekezaji wa moja kwa moja kwa kuwekeza zaidi ya miradi 700 yenye thamani ya dola za Kimarekani (USD) bilioni 7.1 na kutengeneza zaidi ya ajira 87,000 kwa watanzania.

Kwa upande wake Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke amesema China wakati wote ni Rafiki mwaminifu na wa kudumu wa nyakati zote kwa Tanzania na kwamba kutimiza miaka 55 ya urafiki wa nchi hizo ni kielelezo tosha na siku zote wataendelea kuuheshimu na kuuenzi urafiki huo.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamela O'Donnell, ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi na mabalozi waliadili masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha mahusiano, Uwekezaji na Biashara, Afya, Elimu pamoja na Utalii.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam 

Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati wa mazungumzo yao leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan kabla ya kuanza kwa mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuonesha Balozi wa Canada nchini, Mhe. Pamela O'Donnell sheria ya uchaguzi kabla ya kumkabidhi sheria hiyo pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu masuala ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2020


Thursday, October 8, 2020

RAIS MAGUFULI, RAIS CHAKWERA WAWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA MABASI MBEZI

 RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.John Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus Chakwera wameweka jiwe la msingi katika kituo kipya cha mabasi Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam

Kabla ya kuweka jiwe la msingi, Rais Dkt.Magufuli ametoa maagizo, kwa waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kabla ya tarehe 30 Novemba 2020, vinginevyo mkandarasi atakatwa Pesa kwa kuchelewesha mradi.

Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba mabasi 1,000 na teksi 280 kwa siku, Pia kutakuwa na maeneo ya bodaboda na bajaji na na eneo la mamalishe na babalishe.

Mbali na kuweka jiwe la msingi katika kituo cha mabasi mbezi Luis, Rais Chakwera pia ametembelea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Kampuni ya Huduma za Kontena Bandarini (TICTS), Kituo cha Mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center) pamoja na Bandari ya Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiongozana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera mara baada ya kumpokea katika eneo la ujenzi wa stendi mpya ya Mbezi Luis Jijini, Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wakiwa wamesimama huku wakiimba nyimbo za Taifa za mataifa yote mawili kabla ya kuanza rasmi kwa shughuli ya uwekaji wa jiwe la msingi katika maradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Mbezi Luis Jijini, Dar es Salaam




 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipongezana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la maradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Mbezi Luis Jijini, Dar es Salaam



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera kuongea na wananchi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Mbezi Luis Jijini, Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akimuonesha Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera mradi wa ujezi wa Reli ya Kisasa (SGR) wakati alipotembelea mradi huo  Jijini Dar es Salaam 


Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera akiongea na wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa SGR jijini Dar es Salaam. Kushoto mwa Rais Chakwera ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa akifuatiwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwele pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi.


Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera pamoja na mkewe Mama Monica Chakwera wakipokea zawadi kutoka kwa uongozi wa Kituo cha Mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center) wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa SGR jijini Dar es Salaam



Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa, Dkt. Lazarus Chakwera pamoja na mkewe Monica Chakwera wakimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya kuhudumia Makontena Tanzania katika bandari ya Dar es salaam (TICTS), Bw. Horace Hui mara baada ya kutembelea kampuni hiyo leo jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa, Dkt. Lazarus Chakwera akiongea na wananchi pamoja na waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati alipotembela Bandari ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam


 

BALOZI WA TANZANIA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA MFALME WA LUXEMBOURG


 Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji ambaye anawakilisha pia nchini Luxembourg, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme wa Luxembourg, Grand Duke Henri tarehe 2 Oktoba 2020.

Wakati wa hafla hiyo, Balozi Nyamanga na Mfalme Henri walifanya mazungumzo kuhusu umuhimu wa kuongeza wigo wa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi na kutumia ipasavyo fursa mbalimbali zilizopo kwa ajili ya manufaa ya pande mbili. Miongoni mwa maeneo ya ushirikano yaliyojadiliwa ni pamoja na ushirikiano wa anga hususan ndege za mizigo, ushirikiano katika sekta za kifedha na kibenki na sekta ya madini hususan madini ya chuma kama yale ya Mchuchuma na Liganga, eneo ambalo Luxembourg ina uzoefu mkubwa.

Matukio katika Ubalozi wa Tanzania, Abu Dhabi

KUTAFUTA SOLO LA KOROSHO

Mhe. Balozi Mohamed Mtonga alifanya mazungumzo na wafanyabiashara, Bw. Abdo Shamakh Al-Shibani wa kampuni ya SHAFA iliyopo Dubai na Bw. Dzhuraev Khairullo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FoodArt LLC yenye Makao Makuu yake mjini Moscow nchini Urusi. Kampuni ya FoodArt LLC imekuwa ikinunua korosho sehemu mbalimbali duniani na kuziuza katika nchi mbalimbali za Ulaya ikiwamo Urusi.

Mhe. Balozi Mtonga aliwaonesha fursa ya kuweza kununua zao la korosho kutoka Tanzania na kuwapa mwongozo wa ununuzi kama ulivyotolewa na Wizara ya Kilimo na Ushirika na Bodi ya Korosho Tanzania.

Kwa ujumla wafanyabiashara hao walionesha dhamira ya kununua zao la korosho kutoka Tanzania katika msimu huu wa mwaka 2020/2021.

KUKABIDHI UENYEKITI WA SADC

Mhe. Balozi Mohamed Mtonga alikabidhi Uwenyekiti wa SADC Group of Ambassadors hapa Abu Dhabi kwa Balozi wa Nchi ya Msumbiji. Mhe. Balozi Tiago Recibo Castigo. Balozi Tiago, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake kwa mafanikio makubwa katika kipindi chake cha uenyekiti licha ya changamoto ya ugonjwa wa COVID-19.


KUTANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI

Mhe. Mohamed Abdallah Mtonga, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu alifanya mazungumzo na Wakurugenzi wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi (ADNOC), Bw. Khaled Salmeen, Bw. Iman Al Hosani, Bw. Mohamed Al Suwaidi na Bw. Abdulla Al Qubaisi kwa njia ya mtandao (Virtual Meeting).

Balozi alitumia fursa hiyo kuwajulisha fursa kadhaa zilizopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia katika eneo hili la Mafuta na Gesi. Maeneo aliyowajulisha kwa uwekezaji ni yale yaliyohusu uwekaji wa miundombinu katika biashara ya Gesi na Mafuta. Aidha, Balozi aliwajulisha fursa za kibiashara katika biashara ya mbolea aina ya Urea kwa utaratibu wa Bulk Procurement System unaoratibiwa na Tanzania Fertilizers Regulatory Authority na uletaji wa Mafuta kwa pamoja unaoratibiwa na Bulk Procurement System for Petroleum Products. Bidhaa zote hizi huzalishwa na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi (Abu Dhabi National Oil Company (ADNOC).

Vilevile, Balozi aliwasilisha kwa ADNOC miradi ambayo ipo tayari kwa uwekezaji iliyopo katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre) ambayo inatafuta wawekezaji au wabia.

Miradi hiyo ni kama ifuatavyo:

·       Establishment of Strategic Petroleum Reserve Infrastructures (Farm Tanks).

Kwa mujibu wa andiko Mradi utajikita katika ujenzi wa Matanki ya kuhifadhia mafuta katika miji ya Dar Es Salaam, Morogoro, Isaka(Kahama),Makambako, Mbeya, Songwe na Tanga. Watekelezaji wa Mradi huu ni Mwekezaji Mshirika (Strategic Partner) na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development Corporation). 

·       LPG Bulk Distribution Project

Kwa mujibu wa andiko Mradi huu ni kuweka miundombinu ya Kupokea,kuhifadhi na kuweka miundombinu ya kujaza Gesi aina ya LPG. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu katika miji ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Watekelezaji wa Mradi huu ni Mwekezaji Mshirika (Strategic Partner) na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development Corporation).

Kwa upande wao, Wakurugenzi wa ADNOC wamehitaji taarifa mbalimbali ambazo Mhe. Balozi Mohamed Mtonga ameziwasilisha katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kufanyiwa kazi.







 

Wednesday, October 7, 2020

RAIS MHE.DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AMPOKEA MGENI WAKE RAIS WA MALAWI DKT. LAZARUS CHAKWERA JIJINI DAR ES SALAAM

 


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akiongea jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi wakati walipokuwa wakimsubiri Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Terminal 1 Jijini Dar es Salaam. Kushoto mwa Balozi Kijazi ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Terminal 1 Jijini Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera akikagua Gwaride la Heshma lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Terminal 1 Jijini Dar es Salaam 



Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera akizungumza na Wanahabari (hawapo pichani) kutoka Tanzania na Malawi mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wanahabari kutoka Tanzania na Malawi (hawapo pichani) katika mkutano na Waandishi wa Habari mara baada ya mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera


Waziri wa Mabo ya Ndani Mhe. George Simbachawene mwenye (suti ya blue) pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (kushoto) wakiwa pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali wakifuatilia mkutano wa pamoja wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Chakwera wakati walipokuwa wakiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam.








RAIS DKT MAGUFULI AMUANDIKIA BARUA YA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KIONGOZI MPYA WA KUWAIT

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemwandikia barua ya salamu za rambirambi Kiongozi mpya (Amir) wa Kuwait, Mtukufu Sheikh Nawaf Al-Ahmad Al-Sabah kufuatia kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Taifa hilo Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-sabah.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Kuwait hapa nchini amemkabidhi Balozi wa Kuwait Mhe.Mubarak Mohammed Alsehaijan barua iliyoandikwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwenda kwa Kiongozi mpya wa Kuwait.

Prof. Kabudi amesema Tanzania na Kuwait zina mahusiano mazuri sana na muda mrefu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo akitolea mfano wa mfuko wa Kuwait ambao umekuwa wa msaada mkubwa katika kwa Tanzania ambao umekuwa ukisaidia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali hapa nchini ikiwemo barabara.

Ameongeza kuwa msiba wa Kiongozi huyo wa Kuwait ni msiba wa Watanzania wote kwa kuwa kwa muda wote ambao Hayati Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-sabah amekuwa Kiongozi wa Taifa hilo amekuwa karibu sana na Tanzania.


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John akisaini kitabu cha maombolezo katika ubalozi wa Kuwait nchini, kufuatia kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Taifa hilo Mtukufu Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-sabah.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John akimkabidhi Balozi wa Kuwait Mhe.Mubarak Mohammed Alsehaijan barua iliyoandikwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwenda kwa Kiongozi mpya wa Kuwait


 


Balozi wa Kuwait Mhe.Mubarak Mohammed Alsehaijan akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John mara baada ya kumaliza kusaini kitabu cha maombolezo