Friday, February 12, 2021

MKUTANO WA SADC TROIKA WASOGEZA MBELE MKUTANO WA WAKUU WA NCHI

 Na Mwandishi wetu,

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali za Utatu wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC- TROIKA) uliopangwa kufanyika mwezi Machi 2021 umesogezwa mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021 kutokana na changamoto za (Covid 19).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) amesema kuwa mkutano huo umekutana kwa lengo la kupitia na kuridhia mapendekezo ya Mawaziri wa afya wa SADC uliofanyika mwishoni wa mwezi Februari 2021.  

“Awali mawaziri wa Afya wa SADC walipendekeza kuwa mkutano wa Baraza la Mawaziri ufanyike kwa njia ya mtandao pamoja na ule wa Wakuu wa Nchi uliokuwa umepangwa pia kufanyika mwezi Machi usogezwe mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021 kutegemeana na hali ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 itakavyokuwa na kuongeza kuwa mikutano mingine yote itafanyika kwa njia ya mtandao (Video Conference) hadi hapo hali ya maambukizi itakapokuwa imetengemaa,” Amesema Mhe. Ole Nasha

Mkutano wa (SADC TROIKA) umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameeleza kutokana na hali halisi ya kujitokeza kwa kirusi cha Covid 19 kilichojitokeza kusini mwa Jangwa la Afrika imekuwa vigumu kufanyika kwa mkutano huo wa ana kwa ana na badala yake imeamuliwa mkutano huo usogezwe mbele hadi mwezi Mei au Juni 2021.

“Mwezi Januari 2021 Mawaziri wa Afya wa SADC walikutana na kufanya mkutano kwa njia ya mtandao na kufikia maazimio kuwa mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali uhairishwe hadi mwezi Mei au Juni kutegemeana na hali ya COVID 19 itakapokuwa imetengemaa……. ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano wa Baraza la Mawaziri umeridhia kusogezwa mbele kwa mkutano huo,” Amesema Balozi Ibuge

Utatu wa SADC TROIKA kwa sasa unaundwa na nchi za Msumbiji, Tanzania na Malawi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa wa Msumbiji ulipokuwa ukipigwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Utatu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC TROIKA) uliofanyika kwa njia ya mtandao  


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Ole Nasha (Mb) akiandika jambo wakati wa mkutano cha SADC TROIKA) uliofanyika kwa njia ya mtandao


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akichangia mada katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC TROIKA 


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC TROIKA 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.