Tuesday, May 18, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA POLAND, USWISI

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Poland nchini, Mhe. Krzystof Buzalski pamoja na Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri Mulamula amesema kuwa mazungumzo yake na mabalozi hao yalilenga kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uwili (bilateral cooperation) baina ya Tanzania na nchi hizo katika sekta za afya, elimu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.

Akiongelea uhusiano baina ya Tanzania na Poland Balozi Mulamula amesema kuwa wapoland walikuja kwa kasi katika uwekezaji ambapo wana kampuni zao zinazozalisha matreka Kibaha, na kuanzisha miradi katika sekta ya maji, miradi katika uwekezaji wa nafaka pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kitanzania nchini Poland.

“Sasa hivi Balozi amenijulisha kuwa fursa hizo za watanzania kusoma Poland na kutuhamasisha kuzichangamkia fursa hizo, lakini pia tumeongelea jinsi ya kukuza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Poland,” Amesema Balozi Mulamula

Akiongelea kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Uswisi Mhe. Mulamula amesema kuwa ushirikiano wa Tanzania na Uswisi umekuwa ni wa muda mrefu na wamekuwa wakisaidia sana Tanzania katika sekta ya Afya hasa katika kupambana na Malaria.

“……..Uswisi imekuwa ikisaidia mikopo mbalimbali lakini pia ni mwenyekiti mwenza katika kuunganisha Tanzania na nchi wadau/zinzaotoa misaada, pamoja na mambo mengine, madhumuni ya kukutana leo ni kuangalia jinsi gani ya kukuza sekta ya uwekezaji na biashara,” Amesema Balozi Mulamula

Kwa upande wake Balozi wa Poland nchini, mhe. Krzystof Buzalski amesema kuwa wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Poland na Tanzania katika sekta ya uchumi, maendeleo, utalii na siasa.

“Leo tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Poland na Tanzania katika sekta ya uchumi, maendeleo, utalii pamoja na siasa kati ya Poland na Tanzania,” amesema Balozi Buzalski.

Nae balozi wa Uswisi Mhe. amesema kuwa Uswisi na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa siku nyingi kwa zaidi ya miaka 40 na viongozi hawa wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uwili (Bilateral cooperation) katika masuala ya kiuchumi na kisiasa.

“Mimi na Mhe. Waziri tumekubaliana kuendeleza ushirkiano baina ya nchi zetu mbili katika sekta ya afya; elimu; biashara; uwekezaji pamoja na maliasili na utalii,” amesema Balozi Chassot.

Balozi wa Poland nchini, Mhe. Krzystof Buzalski akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimuelezea jambo Balozi wa Poland nchini, Mhe. Krzystof Buzalski katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiteta jambo Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam


Kikao cha Mhe. Waziri Balozi Mulamula na Balozi wa Uswisi kikiendelea 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Chassot pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Uswisi na Wizara ya Mambo ya Nje


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.